Na Issa Mwadangala

Wasafirishaji wa abiria kwa pikipiki (bodaboda) kata ya Mwakakati Tarafa ya Tunduma Wilaya ya Momba Mkoani Songwe, wametakiwa kutumia umoja wao kama chachu ya kuleta maendeleo na ustawi katika jamii zao, badala ya kutumia nguvu vibaya kwa kupiga watu, viongozi wa dini, au kuharibu miundombinu ya serikali.

Rai hiyo imetolewa Desemba 05, 2025 na Polisi kata ya Mwakakati Mkaguzi wa Polisi Robert Kasunga huku akiwasisitiza kuwa vijana hao wana nguvu, afya na kipaji cha kufanya kazi na hivyo wanapaswa kutumia nguvu hizo kujijenga kiuchumi badala ya kupandikiza chuki ndani ya familia na ndugu zao wanaotoka vijijini kwa kuiharibia sifa serikali.

Vilevile, Mkaguzi Kasunga alikemea vitendo vya kutumia pikipiki kubeba watu kwa nia ya kuharibu barabara au miundombinu ikiwa ni pamoja na kupanga vurugu kupitia simu au mitandao ya kijamii, aliwadadavulia kinagaubaga na kuwaweka wazi kuwa tarehe 9 Desemba ni siku ya UHURU wa Tanganyika, siyo siku ya kufanya fujo.

Aidha, Mkaguzi Kasunga amewakumbusha vijana hao kutanguliza uhai na usalama wao kwanza huku akisisitiza kuwa hakuna mtu ambaye maisha yake yamebadilika kwa kufanya vurugu na kuwatania kwa kusema “Hajui hata kama wameletewa suruali mpya baada ya vurugu na maisha hayajabadilika,” amewataka kuwa watulivu na kutii maelekezo endapo kutatolewa maagizo maalum ya kiusalama bila kusukumwa au kulazimishwa.

Mkaguzi Kasunga aliendelea kusisitiza kuwa hatarajii kuona vijana wa kata yake wakikamatwa kwa ajili ya vurugu, wala kuona wazazi wakipigiwa simu kwamba hapa si salama alielezea kuwa, kufanya hivyo ni kupandikiza chuki dhidi ya serikali na jamii na badala yake, amewahimiza vijana hao waendelee kufanya kazi zao kwa kujitafutia kipato na kuendeleza maisha yao ya kila siku.

Pia Mkaguzi Kasunga amewatoa hofu waendesha pikipiki hao kuhusu uwepo wa askari mitaani wakitimiza wajibu wa kulinda raia na mali zao hivyo wao waendelee na kuchapa kazi na wanaofanya kazi za kuchomelea waendelee kuchomelea, na bodaboda waendelee kuwahudumia abiria bila hofu.

Mwishoni, Mkaguzi Kasunga ametoa wito wa kudumisha amani akisisitiza umuhimu wa uhai katika maisha ya ya kila siku ya mwanadamu huku akisema kwa ucheshi kuwa wakati wa vurugu hata nyumbani kwake kulikosa unga kutokana na mashine kufungwa na watoto hawawezi kula wali kila siku, ingawa wanapenda wali ila kwa kipindi hicho walitaka ugali kwahiyo amani ni muhimu, tuihifadhi na kuitunza kwa maendeleo yetu na taifa letu kwa ujumla.