Na Theophilida Felician, JanhuriMedia, Kagera
Washiriki wa imani za asili (Wanandembo) Manispaa ya Bukoba mkoa Kagera wamefanya maombi maalumu ya kuliombea amani taifa na jamii kwa ujumla.
Maombi hayo ya siku moja yamefanyika eneo maalumu linalofahamika Omurulembo lililopo mtaa wa kilimahewa kata Kashai ambapo lengo kuu la maombi hayo ya asili ni kuiombea amani nchi ili iweze kuendelea kuwa na amani na utulivu kama ilivyo siku zote.
Mwenyekiti wa Wanandembo Taifa Mulangi Domina Angribert akiongoza maombi hayo amesema wamefanya maombi hayo kumuomba MweziMungu ashushe Rehema zenye kuiepushia nchi chokochoko zilizoanza kuchomoza kwa ajili yakuididimiza amani yake iliyodumu kwa miaka mingi tangu kupata uhuru.

Mulangi Domina ameendelea kueleza kwamba Tanzania imekuwa jicho ang’avu maeneo mengi duniani kwakudumisha amani, upendo, mshikamano na utulivu hivyo haya mambo yenye kuanzisha vurugu hayana budi kukemewa ili amani iendelee kutawala.
Hata hivyo ameongeza kuwa bila amani ni athari nyingi zinazojitokeza ikiwemo ya mgawanyiko unaopelekea kuteteleka kwa maendeleo, uchumi na jamii kukumbwa na madhira mbalimbali nayenye kuifanya kukukimbia nchi na mengineyo.
Ameongeza kuwa maombi hayo pia yanaigusa serikali inayoongozwa na Mhe Rais dkt Samia Suluhu Hassan kumuombea heri na afya njema ili aweze kuendelea kusimama imara hatimaye kuyashinda majaribu yote yenye nia ovu nakuyumbisha hali ya taswira ya nchi huku akiwasihi wananchi wote kuungana na kushikamana pamoja na kuendelea kuliombea mema taifa hili.

Nao baadhi ya washiriki akiwemo Donatha Pangarace, Chronery Kajumbi, Richard Mushashu na Restidia Limweli Ezironi kwapamoja wamesema maombi hayo ni yenye nia njema hivyo ni imani yao kuwa Mwenyezi Mungu atasimama nao hatimaye aweze kuziepusha husuda, chuki dhidi ya nchi, wametolea mfano wa matukio yaliyotokea hivi karibuni yakihusisha vurugu za maandamano ya tarehe 29 Oktoba siku ya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.
Aidha wametoa wito kwa jamii nzima katu kutokujihusisha na aina yoyote yenye dhamira yakuliangamiza taifa ambapo wamesisitiza kuwa “Mtengo wa panya huwanasa waliomo ndani na wasiokuwemo” hivyo hawanabudi kusimama imara nakuilinda kwa kunguvu zote TANZANIA kwani TANZANIA ni mota tuu haina pacha wake.





