Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kibaha imetenga mamilioni ya fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu katika shule za sekondari, ikiwemo sh.milioni 900 kwa ujenzi wa vyumba vipya vya madarasa na sh. milioni 400 kwa ununuzi wa madawati.

Akizungumza na waandishi wa habari Disemba 10, 2025, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa hiyo, Dkt. Mawazo Nicas, alieleza wamejipanga kikamilifu kuimarisha na kuboresha sekta ya elimu ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi.

Alieleza ,fedha hizo zinalenga kuhakikisha wanafunzi wa kidato cha kwanza wanaotarajiwa kujiunga na masomo mwaka 2026 wanapata madarasa ya kutosha pamoja na samani stahiki, hatua itakayosaidia kuondoa changamoto ya upungufu wa madarasa na madawati.

Dkt. Nicas alisema wanafunzi 6,000 wamefaulu mtihani wa darasa la saba mwaka huu, sawa na asilimia 100, ikilinganishwa na wanafunzi 3,050 waliofaulu mwaka uliopita, hali inayoonesha ongezeko kubwa la ufaulu.

Aliongeza kuwa, ujenzi wa madarasa mapya unatarajiwa kukamilika ndani ya siku 60 ili wanafunzi waanze masomo yao kwa wakati bila changamoto yoyote.

“Kuhusu madawati, mzabuni tayari amepatiwa kazi ya kuyatengeneza ili ifikapo mwaka ujao yawe tayari kwa matumizi ya wanafunzi,” alisema Dkt. Nicas.

Aidha, alisisitiza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekuwa akiwahimiza watendaji kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati, kwa ubora unaostahili na kuendana na fedha zilizotengwa.

“Mimi kama Meya nitasimamia utekelezaji wa miradi hii hatua kwa hatua, na tayari tumeanza kazi,” alibainisha.

Vilevile, aliitaka jamii pamoja na watendaji wa elimu kuhakikisha watoto wote waliofikia umri wa kuandikishwa katika darasa la awali na darasa la kwanza wanasajiliwa kwa mujibu wa taratibu.

“Watoto wote waliofikia umri wa kuandikishwa wataandikishwa ili wapate haki yao ya msingi ya elimu, na hakuna mwanafunzi atakayeachwa nyuma,” alieleza Dkt Nicas.