Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha kufuatilia na kuwachukulia hatua viongozi wote waliojihusisha kuchochea migogoro ya ardhi katika eneo la Lupunga, Kikongo, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.

Kunenge alisema hatua hiyo inalenga kukomesha tabia ya baadhi ya viongozi hasa wa vijiji na mitaa kutumia nafasi zao vibaya kwa kuwahadaa wananchi na kuendeleza migogoro badala ya kusimamia maendeleo.

Akizungumza na wananchi wa Kikongo, Disemba 17, 2025, Kunenge alieleza maamuzi yote kuhusu mgogoro wa ardhi wa shamba namba 9 linalomilikiwa na Lupunga Farm pamoja na shamba namba 30/1 Chekeleni Lupunga yametolewa na Serikali kupitia Tume ya Uchunguzi iliyoanzishwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, hivyo ni lazima yaheshimiwe.

Alieleza kuwa, shamba namba 9 Lupunga lenye ukubwa wa hekari 850 sawa na hekta 341, limegawanywa katika vitalu viwili vya 9/1 na 9/2 kupitia hati namba 32975/1 na 32975/2, na mmiliki halali ni TARIQ SALEH AHMED .

Kutokana na hali hiyo, Kunenge alisema wananchi waliovamia shamba hilo wakidai ni eneo lao la asili wanapaswa kuondoka mara moja kwani wapo kinyume na sheria.

“Ameniagiza Waziri, nami naagiza kila mwenye mamlaka achukue hatua” Waliojihusisha kwa namna moja au nyingine kuchochea migogoro hii huku wakijua maeneo yanamilikiwa kihalali kwa hati za kiserikali, lazima wachukuliwe hatua”

“Tumechoka, badala ya watu kufanya shughuli za maendeleo wanaendeleza migogoro, wanadanganya wananchi na kuwapotezea muda na fedha,” alifafanua Kunenge.

Vilevile, aliagiza viongozi wa Serikali za Mitaa kuacha mara moja kujihusisha na uuzaji wa ardhi, akieleza kuwa tabia hiyo ndiyo chanzo kikubwa cha migogoro ya ardhi mkoani humo.

Kadhalika aliwakumbusha wananchi wajibu wa kujenga kwa kufuata taratibu na kupata vibali vya ujenzi, akisisitiza kuwa ujenzi holela ni kinyume cha sheria.

Kunenge pia aliwahimiza wamiliki wa mashamba na ardhi kulinda mipaka yao na kuendeleza maeneo yao kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.

Akizungumzia mgogoro wa shamba namba 30/1 Chekeleni Lupunga unaohusisha wananchi 214 waliokuwa wakidai fidia kutoka kwa kampuni ya Transcontinental Forwarders Ltd kuwa ni wamiliki wa asili, Kunenge alibainisha Tume ya Uchunguzi imebaini ilikuwa kifuta jasho na si fidia.

“Tume imebaini kuwa Transcontinental Ltd ni mmiliki halali wa shamba hilo kwa umiliki , walilipata kihalali, hivyo waendelee na shughuli zao za uwekezaji,” alieleza Kunenge.

Hata hivyo, Tume imeielekeza kampuni hiyo kutoa eneo kwa wakazi hao, kila mwananchi akitengewa mita za mraba 500 kwa ajili ya makazi, huku kampuni ikigharamia upimaji wa mchoro na wananchi kugharamia umilikishwaji wa hati.

Migogoro hiyo imekuwa ikifuatiliwa tangu enzi za mawaziri wa zamani wa Ardhi akiwemo William Lukuvi na Angelina Mabula, kisha Jerry Silaa ambaye aliunda Tume hiyo, kazi imekamilika na Waziri wa sasa na Serikali imetoa maamuzi ambayo yamewasilishwa kwa uongozi wa Mkoa wa Pwani kwa utekelezaji.