Serikali ya Indonesia imeahidi kutimiza ahadi yake ya kumalizia utoaji wa kiasi cha fedha za msaada kilichosalia kwa ajili ya kukamilisha ukarabati wa Kituo cha Mafunzo ya Wakulima Vijijini (FARTC) kilichopo Mikindo mkoani Morogoro.

Ahadi hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa wa Maendeleo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Indonesia, Bi. Rina Setyawati alipokutana kwa mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Macocha Tembele Desemba 17, 2025.

Mazungumzo hayo ambayo yalihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Afrika wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Indonesia, Bi. Dewi Justicia Meidiwaty, Indonesia imeihakikishia Tanzania kuwa itaendelea kutoa fursa za ufadhili wa masomo (scholarships) pamoja na programu maalumu za kuwajengea uwezo watumishi wa Serikali katika sekta mbalimbali za kipaumbele.

Kwa upande wake, Balozi Tembele aliishukuru Serikali ya Indonesia kwa misaada inayoipatia Tanzania ikiwa ni pamoja na ufadhili wa masomo na mafunzo ya kuwajengea uwezo Watanzania. wakiwemo watumishi wa umma katika sekta za kimkakati.