Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tabora

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo amewataka wahitimu wa chuo cha ardhi Tabora (ARITA) kuingia kwenye dunia ya kazi kwa moyo wa uadilifu, uzalendo na ubunifu.

Amesema, Taifa linawategemea wahitimu hao sambamba na kuhitaji wataalamu wanaoweza kutumia elimu kwa manufaa ya wote na si kwa maslahi binafsi.

“Tumieni utaalamu wenu kwa weledi, uadilifu na kufuata sheria. Epukeni kabisa mambo ya rushwa na ufisadi”. Amesema.

Mhe. Dkt Akwilapo ametoa kauli hiyo leo tarehe 19 Desemba 2025 katika Mahafali ya 43 Chuo cha Ardhi Tabora (ARITA) yaliyofanyika chuoni hapo mkoani Tabora.

Aidha, amewataka wahitimu hao wa chuo cha ARITA kuendelea kujifunza kwa kuwa elimu haina mwisho na kusisitiza kuwa anataka kuona elimu waliyoipata inakuwa na manufaa kwa Taifa na sio machungu kwa Taifa.

“Muwe mabalozi wema wa Chuo. Msidanganyike na yanayoandikwa kwenye mitandao kwamba nyie ni kundi la wanajamii wenye ukaidi, wasio na utii, wala heshima kwa wazazi, viongozi na Serikali, Nyinyi ni hazina ya Taifa”. Amesema.

Mkuu wa wilaya ya Tabora Bi. Upendo Wella amewataka wahitimu wa chuo hicho kutumia vizuri utaalamu na ujuzi walioupata kwa kushirikiana na jamii katika kutatua changamoto za sekta ya ardhi.

“Wahitimu kama hamna ajira mkajiunge katika vikundi na muanzishe shughuli,elimu mliyopata mkaitumie vyema”. Amesema

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Ardhi Tabora Dkt Lucy Shule amesema, chuo hicho kinaendelea kufanya maboresho mbalimbali yatakayokiwezesha chuo kuwa na miundombinu ya kisasa ya kufundishia na kujifunza.

Kwa mujibu wa Dkt Shule, maboresho hayo yatakiwezesha chuo cha Ardhi Tabora kuwa na uwezo wa kuongeza udahili na kozi mpya.

Mkuu wa chuo cha Ardhi Tabora Bw. Jeremiah Minja amesema, chuo chake ni miongoni mwa vyuo vichache nchini vinavyotoa mafunzo ya uchapishaji wa nyaraka nchini.

“Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya kazi za uchapishaji katika ngazi ya Wizara na wateja wengine na kutokana na Wizara kukipa Chuo mtambo mkubwa wa uchapishaji uliopo Dar es Salaam chuo kina nia ya kuanzisha karakana nyingine ya uchapishaji katika Jiji la Dar es Salaam”.Amesema Bw. Minja.

Katika risala yao iliyosomwa na Yohana Mhendi wahitimu wa chuo hicho wameishukuru Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuboresha mazingira ya chuo ikiwemo miundombinu ya kujifunzia kama vile kumbi za Mihadhara na Maktaba.

Katika mahafali hayo ya 43 ya chuo cha Ardhi Tabora, jumla ya wanafunzi 688 walihitimu ambapo kati ya hao kozi za Sanaa, Ubunifu na Uchapishaji ni 28, Kozi za Urasimu Ramani ni 126, Kozi za Usimamizi wa Ardhi, Uthamini na Usajili ni 483, Kozi za Usimamizi wa Mazingira ni 22 na Kozi za Mfumo wa Taarifa za Kijiografia ni 29.