Na Mwandishi Wetu, Morogoro 

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) imeweka mkakati maalum wa kuandaa na kusambaza ripoti za ukaguzi katika mfumo wa nukta nundu (Braille), hatua inayolenga kuhakikisha watu wenye ulemavu wa uoni hafifu wanapata haki sawa ya kufikia na kuelewa taarifa za ukaguzi wa matumizi ya rasilimali za umma.

Hayo yameelezwa na Mchumi Mwandamizi wa NAOT, Emanuel Lazaro wakati akiwasilisha mada kuhusu njia na aina za ukaguzi katika mafunzo ya ukaguzi kwa waandishi wa habari yaliyofanyika mkoani Morogoro yaliyoandaliwa na Ofisi hiyo.

Emanuel alisema mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa NAOT unaolenga kuimarisha uwajibikaji, uwazi na ushirikishwaji wa wadau wote katika mchakato wa ukaguzi, ikiwemo makundi maalum kama watu wenye ulemavu.

Alisema katika mpango mkakati Ofisi hiyo imejipanga kuandaa taarifa za ukaguzi ambazo ni rafiki na zinazoweza kufikiwa na kila mmoja, wakiwemo watu wenye uoni hafifu kupitia matumizi ya nukta nundu.

“Miongoni mwa vipaumbele vyetu ni kuhakikisha ripoti za ukaguzi zinawafikia wadau wote bila ubaguzi. Kwa sasa NAOT imeanza mchakato wa kuandaa ripoti za nukta nundu ili kuwawezesha watu wenye uoni hafifu kusoma na kuelewa taarifa hizo,” alisema Emanuel.

Aliongeza kuwa lengo la kuandaa ripoti hizo ni kuwawezesha watu wenye ulemavu wa uoni hafifu kufahamu kile alichokibaini Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ukaguzi pamoja na mapendekezo yanayotolewa kwa Serikali.

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya CAG, Charles Kichere, Mkaguzi Mkuu wa Nje (CEA) wa mkoa wa Morogoro, Baraka Mfugale, alisema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi unaolenga kuimarisha ushirikishwaji wa wadau, hususan vyombo vya habari.

Mfugale alisema mpango huo unatambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari kama kiungo kati ya taarifa za ukaguzi na wananchi, kwa kuwa vina jukumu la kuzichambua, kuzifafanua na kuzifikisha kwa umma kwa lugha rahisi na inayoeleweka.

Alisema NAOT itaendelea kuboresha uwazi katika utoaji wa taarifa za ukaguzi, kuimarisha mawasiliano na wadau, pamoja na kujenga uelewa mpana kuhusu majukumu, kazi na mipaka ya Ofisi hiyo.

“Mafunzo haya ni uthibitisho wa dhamira ya NAOT katika kuwawezesha waandishi wa habari kusoma, kuchambua na kuripoti kwa usahihi ripoti za CAG, jambo linalosaidia kuimarisha uwajibikaji wa umma,” alisema Mfugale.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa NAOT, Focus Mauki, alisema Ofisi inaamini mafunzo hayo yatawawezesha waandishi wa habari kuuliza maswali ya kitaalamu, kufanya uchambuzi wa kina na kuibua mijadala chanya itakayosaidia Serikali, Bunge na taasisi nyingine kuchukua hatua stahiki kulingana na mapendekezo ya ukaguzi.

Mauki alisema mafunzo hayo yametolewa kwa waandishi wa habari, Asasi za Kiraia na makundi mbalimbali katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Shinyanga, Mtwara, Tanga, Kilimanjaro, Manyara, Tabora, Iringa, Ruvuma, Lindi, Rukwa, Njombe, Mbeya, Mwanza, Mara, Dodoma, Pwani na Morogoro.

“Kwa Morogoro, mafunzo haya ni mwendelezo wa juhudi za kuhakikisha waandishi wa habari wa mikoa yote wanapata uelewa sawa kuhusu kazi za ukaguzi na matumizi sahihi ya ripoti za CAG katika kuimarisha uwajibikaji wa umma,” alisema Mauki.