Wenyeji wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, Morocco, wameanza kampeni yao ya kutafuta taji la pili la barani Afrika  kwa ushindi wa mabao 2 – 0 dhidi ya Comoros katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa  mjini Rabat.

Atlas Lions walipoteza nafasi nzuri ya kuongoza dakika ya 11 baada ya Iyad Mohamed kumwangusha Brahim Diaz ndani ya eneo la hatari, lakini kipa wa Comoros Yannick Pandor aliokoa mkwaju wa penalti wa Soufiane Rahimi kwa goti lake la kushoto.

Wawakilishi wa visiwa vya Bahari ya Hindi Comoros walikaa nyuma na kuwakwaza wapinzani wao hadi dakika 10 za kipindi cha pili, pale Diaz aliachwa bila ulinzi karibu na eneo la penalti na akapachika mpira uliopigwa chini na Noussair Mazraoui kuvuka boksi.

Bao la mchezaji huyo wa Real Madrid lilipokelewa kwa shangwe kubwa na wengi wa mashabiki 60,180 waliokuwapo katika Uwanja wa Prince Moulay Abdellah. Baada ya hapo mchezo ulipamba moto, ambapo mshambuliaji wa Comoros Rafiki Said alizuiwa na miguu ya kipa Yassine Bounou, huku Pandor akiokoa kwa ustadi jaribio zuri la Mazraoui.

Mchezaji wa akiba Ayoub El Kaabi alifunga bao la kuvutia kwa shuti la mkasi (overhead kick) dakika 15 kabla ya mwisho, akaihakikishia Morocco ushindi na kuthibitisha matarajio ya kabla ya mechi kwa kikosi cha Walid Regragui.

Morocco ilipata ushindi huo bila nahodha wao muhimu Achraf Hakimi, ambaye alikuwapo benchi pekee baada ya kupata jeraha la kifundo cha mguu alipokuwa akiichezea Paris St-Germain kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa mapema Novemba. Pia walimpoteza beki wa kati Romain Saiss mapema kutokana na jeraha.

Pointi tatu hizo ziliifanya Morocco kuongeza rekodi yao ya dunia ya ushindi mfululizo hadi mechi 19, ingawa mtihani mgumu zaidi unawasubiri dhidi ya Mali siku ya Ijumaa (20:00 GMT).

Leo Jumatatu kutakuwa na mechi tatu, ambapo timu za Afrika Magharibi zitakutana na Zambia katika mchezo wa pili wa Kundi A, huku Misri na Afrika Kusini zikianza kampeni zao katika Kundi B.

Morocco imekuwa timu ya juu zaidi Afrika katika viwango tangu Kombe la Dunia la FIFA 2022, walipokuwa timu ya kwanza kutoka bara hilo kufika nusu fainali. Malengo yao uwanjani yameambatana na uwekezaji mkubwa katika viwanja na miundombinu ya soka, vyote vikidhaminiwa na Mfalme Mohammed VI.