Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amewataka Wanakagera wanaoishi nje ya Mkoa wa Kagera kurejea nyumbani kuwekeza, akisisitiza kuwa maendeleo ya mkoa huo yanahitaji ushiriki wa wadau wote, hususan wananchi wenye asili ya Kagera waliopo maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Waziri Simbachawene ametoa wito huo wakati wa hafla ya kufunga Tamasha la Utamaduni la Ijuka Omuka lililofanyika katika Uwanja wa Kaitaba, Manispaa ya Bukoba, Desemba 21 mwaka huu. Tamasha hilo lililenga kuwaunganisha Wanakagera wote kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Amesema tamasha hilo ni jukwaa muhimu la kuwakutanisha Wanakagera, kujadili mustakabali wa maendeleo yao na kuweka msingi imara wa urithishaji wa maadili, mila na desturi kwa kizazi kipya.

Aidha, Waziri Simbachawene amewataka wazazi nchini kuhakikisha wanawafundisha watoto wao mila, desturi na utamaduni wa asili, ili kuepusha vijana kujiingiza katika mienendo isiyofaa inayoweza kuhatarisha maadili ya jamii.

Katika hatua nyingine, amewashauri Wanakagera kuwekeza katika kilimo chenye tija, hususan zao la ndizi na bidhaa zitokanazo na zao hilo, huku akiwahimiza pia kufanyika kwa utafiti wa kitaalamu ili kubaini aina bora za ndizi zinazoweza kuzalishwa kwa wingi na kusafirishwa nje ya nchi. Hatua hiyo itasaidia kukuza uchumi wa Mkoa wa Kagera na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Hajat Fatma Mwassa, amesema lengo kuu la Tamasha la Ijuka Omuka ni kuirudisha Kagera kwenye uhalisia wake wa kitamaduni, pamoja na kujadili maendeleo ya mkoa, kuibua fursa zilizopo na kuweka mikakati ya kutatua changamoto zinazoukabili mkoa huo.

Amesema tamasha hilo limekuwa chachu ya mshikamano, majadiliano ya maendeleo na uhifadhi wa utamaduni wa Wanakagera, huku akitoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kuliunga mkono ili liwe endelevu.

Tamasha la Ijuka Omuka linatarajiwa kuwa tukio la kudumu litakalotumika kama jukwaa la utamaduni, uchumi na maendeleo ya kijamii kwa Wanakagera waliopo ndani na nje ya nchi.

Ikumbukwe kuwa Tamasha la Ijuka Omuka ni awamu ya tatu kufanyika ndani ya Mkoa wa Kagera, likiwa limewakutanisha Wanakagera kutoka sehemu mbalimbali duniani na kubeba kaulimbiu isemayo: “Wekeza Kagera, irudishe katika ubora wake.”