Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Zanzibar

Tanzania imepitia mtikisiko. Matukio ya Oktoba 29, 2025 na siku chache zilizofuatia, yameweka doa katika siasa za Tanzania.

Haikupata kufikirika kuwa Tanzania hii watu wangechoma moto magari, nyumba za watu na serikali, vituo vya mafuta au watu wangepigwa risasi katika maandamano yaliyogeuka vurugu.

Sitanii, kila ninayezungumza naye amepigwa butwaa. Mimi nilikuwa mmoja wa watu ambao niliamini mitandao ya kijamii haiwezi kuchochea vurugu zikatokea. Lakini kwa hakika, zamu hii kila awaye ameshuhudia jinsi mitandao ya kijamii ilivyotumiwa na watu wasiozidi watano kuchochea vurugu katika nchi yetu.

Niseme bayana kuwa binafsi katika yote, nilichagua kupigania amani. Kupitia maandiko yangu, mijadala katika redio na televisheni, nilionya kuwa hatuna sababu ya kuzalisha machafuko yatakayopoteza maisha na mali. Nilisema mara kadhaa kuwa tukifanya vurugu tukauana, bado tutatafuta wasuluhishi kuturejesha hapa tunapotaka kutoka.

Unabii huu umetokea. Zimefanyika vurugu, sasa zinasikika sauti za fulani anaweza kutusuluhisha. Sijabadili msimamo. Najua Rais Samia Suluhu Hassan wakati anazungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam alizungumza sentensi fupi ambayo sina uhakika kama tumeifikiria na kuichambua kwa kina.

Rais Samia alisema kwa wanaotaka urais wa mwaka 2030 wakae kando. Akasema bora wafanye siasa hizo wakiwa nje ya serikali. Kwa hakika baada ya kauli hiyo nimefuatilia. Nimekutana na kitu kinaitwa TK Movement.

Nimesikiliza, nikatajiwa wahusika na malengo yao, hakika nimebaki kinywa wazi.

Sitanii, leo niseme jambo ambalo sijawahi kulisema hadharani. Jambo hili nimepata kulizungumza na viongozi kadhaa. Nasema si lazima sisi sote tuwe madiwani, wabunge au marais. Kila mtu atimize wajibu wake katika nafasi aliyopo. Najua wapo watu wana kiu ya kuwa mawaziri, wabunge, madiwani au Rais, ila binafsi naamini nyadhifa hizi zinakuja kwa mkono wa Mungu si lazima tuzipiganie.

Mimi, Deodatus Balile, naamini kila mtu akitimiza wajibu wake vizuri katika nafasi aliyonayo, nchi hii itapiga hatua kubwa. Kila awaye ajipime alipo, aone kama anatimiza wajibu wake. Tulikwepe wimbi la kutafuta urais usiku na mchana, kwani Mungu pekee ndiye awezaye kusema nani awe Rais na nani asiwe.

Mimi mwandishi wa habari niandike habari zenye tija na maendeleo kwa jamii, mwalimu afundishe vema wanafunzi, katibu kata afanye kazi ya kusuluhisha na kuongoza wananchi, mganga, tabibu au daktari atibu wagonjwa, mhandisi ajenge barabara bila kuiba lami au vifusi, fundi rangi au majenzi asiibe saruji au misumari.

Nesi amhudumie mgonjwa kwa upendo. Padri au Kasisi, Mchungaji au Nabii ahubiri neno la Mungu. Polisi afanye kazi ya kukamata wahalifu, si kuwabambikia kesi. Trafiki atende haki barabarani. TRA na watoza ushuru wasitishie watu kufunga biashara bali wawaongoze kukuza biashara, wanafunzi waongeze bidii katika masomo badala ya kutamani kuacha shule kuwa madiwani au wabunge.

Mama Ntilie ahakikishe haunguzi chakula, bodaboda ahakikishe hapiti taa nyekundu au kupita kushoto kwa magari bila kuwaza juu ya roho yake na familia yake. Tujitambue, tujue kuwa umiliki wa mali unaendana na umri na muda wa kufanya kazi.

Mwanafunzi asiseme anataka kumiliki V8, ilhali anasomeshwa shule bure na kulipiwa ada kwa njia ya mkopo akiwa chuo kikuu na stahiki yake ni kupata Asโ€ฆ
Viongozi wenye nafasi waache kupikiana majungu, kwa maana ile migogoro tunayoisikia Katibu Mkuu asimtunishie msuli Waziri au Mkurugenzi akawakaangia sumu anaoona ni washindani wake tarajiwa. Fundi bomba aumie moyoni kuona maji yanamwagika kwa maana ya bomba kupasuka, fundi chereani asipokee nguo za wateja 10 ilhali akijua ana uwezo wa kushona nguo moja kwa siku.

Sitanii, tusiseme uongo au kushuhudia yasiyo ya kweli. Tunene yale tu tunayoweza kuyathibitisha. Tuache roho mbaya, kwamba serikalini au sekta binafsi ukisikia mwenzako kuna mpango wa kumpandisha cheo unatafuta oko ukazibe.

Jirani asinunue gari ukachimba shimo njiani litumbukie, mwanafunzi asishinde mtihani ukaenda kwa sangoma aheuke! Eti unamtumia mapepo!
Sijui leo mnanielewa? Rafiki yako asinunue maziwa, akatoka nje kwenda uani kabla hajamaliza kuyanywa ukatemea mate. Haikusaidii kitu. Badala ya kuwaza uchawi, waza uganga.

Badala ya kuchimba mashimo, jenga madaraja. Badala ya chuki, jenga upendo. Badala ya roho ya korosho, azimia kuwa kuanzia leo utasaidia kila awaye ilimradi imo ndani ya uwezo wako.

Mrudie Mungu kama ulipata kupotea. Ukiwa Mhariri, furahi kuona habari ya mwandishi wako imetoka, badala ya kusema amepata mshiko ngoja nisiitoe akome. Watanzania tuhame kutoka kwenye lindi la michango ya harusi ambayo sasa single ni Sh 99,000 na double ni Sh 100,000. Kuna harusi za Sh milioni 80, wakati unaweza kujenga kiwanda cha kuzalisha misumali kwa Sh milioni 35.

Watanzania tuanze kuonyeshana fursa. Wanaotutumia kuandamana kuchoma magari, nyumba na kupigwa risasa, wanaishi ughaibuni. Kila tunavyozidi kuuana wao wanazidi kupewa misaada mipya.

Nchi yetu haitajengwa kwa kushitakiana kwa Wazungu. Kauli chafu na za kudharauliana kumwita Rais Mama Abdul, badala ya jina lake halisi la Rais Samia hazituongezei shibe.

Hivi tumefikaje hapa? Ni mitandao au mihemko?
Sitanii, mnyukano wa kisiasa uliotikisa mioyo ya wengi unaonekana kufikia tamati. Joto la maneno limepungua, hekaheka za mitaani zimenyamaza, na nchi inahitaji kurejea katika mstari wake wa kawaida: kufanya kazi. Huu si wakati wa kujikunja, bali wa kukunjua, kunyoosheana mikono. Taifa linaitazama serikali, likisubiri ishara thabiti kwamba ukurasa mpya umefunguliwa na safari ya utekelezaji imeanza kwa kasi.

Dalili njema tayari zinaonekana. Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, ameonyesha kwa vitendo maana ya uongozi unaokwenda na muda. Anasikiliza, anatembelea miradi, anatoa maelekezo, na muhimu zaidi – anasimamia. Huu ndio mfano unaohitajika kuigwa. Uongozi unaosukuma kasi, si unaosubiri upepo. Vivyo hivyo, Waziri wa Maendeleo ya Vijana, Dk. Joel Nanauka, ameonekana kuwa karibu na vijana, akizungumza lugha yao (meme) na kuunganisha sera na fursa halisi. Hapa ndipo matumaini ya kizazi kipya yanapopata pumzi.

Sitanii, kwa vyovyote iwavyo taifa haliwezi kusimama kwa juhudi za wachache. Mawaziri wote wanapaswa kuchangamka. Tunahitaji kasi ile ile tunayoiona kwa Waziri wa Ujenzi, Abdallah Hamis Ulega – kila barabara iwe hadithi ya maendeleo, kila daraja liwe ishara ya kuunganisha uchumi na matumiani ya watu.

Tunahitaji kasi na uthubutu wa Waziri wa Nishati tunaouona kupitia TANESCO wa kuzindua โ€˜smart meterโ€™. Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO Lazaro Twange na Waziri wa Nishati Deogaratias Ndejembe wamethubutu. Leo tuna umeme wa uhakika, na gharama ziwe rafiki kwa viwanda na kaya. Haya si mapambo ya maneno; ni misingi ya uchumi unaokua.

Ni wakati wa kuwasikia mawaziri kila kona ya nchi. Kutoka vijijini hadi mijini, kutoka mipakani hadi katikati ya miji, sauti ya serikali isikike ikisimamia utekelezaji wa Ilani. Ziara zisije kuwa za picha, bali ziwe za kazi. Ripoti zisitulize vichwa tu, bali zionyeshe matokeo. Wananchi wanataka kuona – si kusikia – mabadiliko.

Sitanii, Rais Samia Suluhu Hassan aliweka bayana dira yake kuwa siku 100 za mwanzo wa uongozi wake wa kipindi cha pili cha Awamu ya Sita ataleta matokeo ya haraka. Huu ni mtihani wa nidhamu, uratibu na uwajibikaji. Kila wizara iwe na malengo yanayopimika, muda maalumu, na taarifa za wazi. Kila mradi ufanisi au ucheleweshaji wake uelezwe, na kila mafanikio yaonekane. Serikali iendeshe kazi kama timu moja, si visiwa vilivyotengana.

Baada ya mnyukano, busara imetawala. Busara hii isigeuke usingizi. Igeuke kazi. Taifa lina rasilimali, lina watu, na lina matumaini. Kinachohitajika sasa ni kasi ya utekelezaji, ufuatiliaji makini, na uongozi unaosikika na kuonekana. Tukifanya hivyo, ndani ya siku 100, Watanzania wataanza kuona mwanga – na kuamini tena kwamba serikali imo kazini, si kwenye maneno.

Tusiendelee kutafuta mchawi, bali tuchape kazi kwa maendeleo ya nchi yetu. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404 827