Mradi wa utafiti wa mafuta na gesi wa Eyasi–Wembere unaendelea kuwa mfano bora wa jinsi Tanzania inavyotumia rasilimali zake kwa manufaa ya wananchi. Kupitia awamu ya pili ya mradi huu unaotekelezwa Kijiji cha Endeshi, wilayani Karatu, zaidi ya Watanzania 2,000, wengi wao vijana wa maeneo ya jirani, wamepata ajira za moja kwa moja.

Huu ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali zao. Katika hatua ya utafiti, kazi hii inafanywa na kampuni ya Kitanzania, Africa Geophysical Services (AGS), jambo linaloipa kipaumbele ajira za wazawa na fursa kwa watoa huduma wa ndani.

Mbali na kuongeza kipato na kuchochea uchumi wa wananchi na maeneo husika, mradi huu pia unajenga uwezo wa kitaalamu kwa Watanzania. Vijana wanaoshiriki wanapata ujuzi na uzoefu muhimu unaowawezesha kushindana katika soko la ajira la kimataifa na kusaidia nchi kusimamia rasilimali zake kwa ufanisi zaidi.

Mradi wa Eyasi–Wembere unaendeshwa chini ya usimamizi wa PURA, kuhakikisha unazingatia sera na sheria za nchi, hususan utekelezaji wa sera ya Local Content. Kupitia miradi kama hii, Tanzania inaendelea kujenga msingi imara wa kuhakikisha rasilimali zake zinawanufaisha wananchi na taifa kwa ujumla, sasa na kwa vizazi vijavyo.