Na Mwandishi Wetu
KLINIKI ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) tawi la Oysterbay imeendelea kung’ara katika utoaji wa huduma bora za kibingwa za moyo, baada ya kufikia mafanikio makubwa kwa kuhudumia hadi wagonjwa 900 kwa mwezi ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake.
Kliniki hiyo iliyopo katika jengo la Oysterbay Plaza, barabara ya Ali Bin Said jijini Dar es Salaam imekuwa kivutio kwa wagonjwa wengi kutokana na miundombinu ya kisasa, huduma zenye ubora wa hali ya juu pamoja na kupungua kwa foleni za kusubiri huduma za kitabibu.
Akizungumza leo na waandishi wa habari wakati wa maadhimisho ya mwaka mmoja wa kliniki hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge alisema ongezeko la wagonjwa linaakisi imani kubwa ya wananchi kwa huduma zinazotolewa na taasisi hiyo.
“Awali tulianza na idadi ndogo ya wagonjwa, lakini sasa tunahudumia wastani wa wagonjwa 225 kwa wiki. Mafanikio haya yametokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya afya ambao umewezesha wananchi kupata matibabu bora hapa nchini badala ya kusafiri nje,” alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Moyo na msimamizi wa kliniki hiyo Smita Bhalia alisema kliniki hiyo ilianza kuhudumia wagonjwa wapatao 250 kwa mwezi lakini sasa imeongeza wigo wa huduma na kufikia wagonjwa 900 kwa mwezi.
“Tunatoa huduma za magonjwa ya moyo, ushauri wa lishe bora, mazoezi tiba (fiziotherapia) pamoja na elimu ya afya kwa jamii. Lengo letu ni kuboresha na kuimarisha afya ya wananchi kwa ujumla,” alisema Dkt. Smita.
Wagonjwa wanaopata huduma katika kliniki hiyo kutoka ndani na nje ya nchi wameeleza kuridhishwa na huduma zinazotolewa, hususan mfumo wa miadi mtandaoni na matumizi ya bima za afya.
“Huduma hapa ni nzuri sana, utolewaji wa dawa ni wa haraka na hakuna foleni ndefu,” alisema Margareth Komba, mkazi wa Dar es Salaam.
Naye Louis Manzombi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alisema wataalamu wa moyo tawi la JKCI Oysterbay wanatoa huduma bora. Amekutana na Dkt. Kisenge na wataalamu wengine, wamemuhudumia vizuri kwa weledi mkubwa.

