Na Mwamvua Mwinyi, JamhutiMedia, Pwani
MKAKATI wa Serikali wa kuvutia uwekezaji na kuzalisha ajira unaendelea kuzaa matunda mkoani Pwani, baada ya mkoa huo kuibuka kinara kitaifa kwa kuzalisha ajira 86,621, hatua iliyomfanya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Alexander Mkumbo, kuipongeza kwa utekelezaji mzuri wa vipaumbele vya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Profesa Mkumbo alitoa pongezi hizo , wakati wa hafla ya makabidhiano ya hati za mikataba ya uwekezaji kwa wawekezaji waliopatiwa maeneo katika Eneo Maalum la Uchumi la Bagamoyo Eco Maritime City (BEMC SEZ) pamoja na kutolewa kwa taarifa ya hali ya uwekezaji nchini kwa mwaka 2025.

Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Mkumbo alieleza, Mkoa wa Pwani umeonyesha mfano wa kuigwa kwa kuongoza kitaifa katika kipaumbele cha uzalishaji wa ajira.
Alieleza, mafanikio hayo ni matokeo ya mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, hongera sana, Mkoa wa Pwani ndio kinara katika utekelezaji wa kipaumbele cha Mheshimiwa Rais cha uzalishaji wa ajira hapa nchini,” alisema Prof. Mkumbo.
Kwa upande wa miradi ya uwekezaji, alisema Mkoa wa Pwani umeshika nafasi ya pili kitaifa kwa kuwa na miradi 208, huku Mkoa wa Dar es Salaam ukiongoza kwa idadi kubwa ya miradi ya uwekezaji nchini.

Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Gilead Teri, alifafanua makampuni yaliyokabidhiwa hati za mikataba ya uwekezaji ni Canary Industrials Limited, Grosso Engineering and Fabricators Limited, Jaribu Cashews Production Limited, Novara Global Steel, Shah Steel Global na MCGA Auto Limited.
Alisema uwekezaji wa makampuni hayo unajikita katika sekta zenye mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa, ikiwemo viwanda vya chuma, usindikaji wa mazao ya kilimo,sanjali na sekta ya magari na huduma zake, ambazo zinatarajiwa kuongeza ajira na kuchochea uchumi.





