Na Allan Kitwe, JamhuriMedia,Tabora
WATU wawili wamepoteza maisha kwa kupigwa na radi wakiwa wamejikinga mvua kwenye kibaraza cha nyumba yao iliyoegemewa na mti katika Kijiji cha Songambele, Kata ya Uyowa, Wilayani Kaliua Mkoani hapa.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani hapa SACP Richard Abwao amethibitisha kutokea tukio hilo Desemba 27 mwaka huu na kuongeza kuwa mbali na waliopoteza maisha watu wengine wawili walijeruhiwa pia.
Ametaja waliopoteza maisha kuwa ni Mwagala Marando (19) na Moses Lwega (20) wakulima, wakazi wa kijiji hicho na waliojeruhiwa ni Yohana Peter (18) na George Deusi (18), na wanaendelea kupatiwa matibabu kwenye kituo cha afya.
Kamanda Abwao ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari hasa katika kipindi hiki ambapo mvua zimeendelea kuongezeka na kuwataka wajikinge katika maeneo yaliyo salama ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.
Wakati huo huo, mwili wa mwanaume mmoja aliyefahamika kwa jina la Hamis Ramadhan, mkazi wa Kata ya Isevya, dereva wa bodaboda, umeokotwa katika mtaro wa maji machafu uliopo Mtaa wa Malolo katika Manispaa ya Tabora.
Kamanda Abwao ameeleza kuwa uchunguzi wa kisayansi unaendelea kufanyika ili kubaini chanzo cha kifo hicho na watatoa taarifa kwa umma, mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete.
Mbali na uchunguzi huo amesema kuwa jitihada za kupata pikipiki hiyo pia zinaendelea kwa kuwa ulionekana mwili tu bila pikipiki aliyokuwa akiendesha, aliomba wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili kufanikisha uchunguzi na kupatikana pikipiki hiyo.


