Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
WANANCHI wa Kata ya Misugusugu, Manispaa ya Kibaha, wamelalamikia uchafuzi mkubwa wa mazingira unaotokana na maji machafu yanayotiririshwa na baadhi ya viwanda, ikiwemo Kiwanda cha karatasi cha Fortune Paper, hali iliyolazimu manispaa kusimamisha shughuli za kiwanda hicho ndani ya wiki moja kufuatia agizo la Meya wa Manispaa hiyo, Dkt. Nicas Mawazo.
Malalamiko hayo yalitolewa wakati wa ziara ya Meya wa Manispaa ya Kibaha katika kata hiyo, ambapo wananchi walieleza kuwa maji yenye kemikali hutiririshwa kutoka viwandani hususan kipindi cha mvua, na kusababisha madhara ya kiafya ikiwemo kuwashwa miili na kuungua miguu.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Diwani wa Kata ya Misugusugu, Ally Simba, alieleza changamoto ya maji taka kutoka viwandani imekuwa kubwa na kuathiri moja kwa moja makazi, mashamba na afya za wananchi.

Alieleza kuwa, Serikali kupitia Ilani ya CCM imejipanga kuweka mifumo ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira ili kupunguza au kuondoa kabisa athari kwa wananchi.
“Kata hii inaongoza kwa uwepo wa viwanda, tunaomba wawekezaji wahakikishe wanazingatia mifumo sahihi ya maji taka na kuacha kutiririsha maji yenye kemikali hasa kipindi cha mvua kwani yanaathiri mashamba na makazi ya wananchi,” alisema Simba.
Simba aliwahakikishia wananchi kuwa ataendelea kusimamia kero zao pamoja na kuhakikisha shughuli za kiuchumi zinaendelea kwa kuzingatia sheria na kulinda mazingira ya Kata ya Misugusugu.
Mkazi wa Misugusugu, Mataba Matiku, alisema maji machafu yanayotiririshwa na baadhi ya viwanda yamesababisha kuungua miguu yake, akiiomba Serikali kuchukua hatua madhubuti ili kurejesha imani ya wananchi kwa Manispaa na Serikali kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Saeni, Edward Kitale, alitaja baadhi ya viwanda vinavyolalamikiwa kuwa ni pamoja na kiwanda cha sabuni, Kiwanda cha karatasi cha Fortune Paper pamoja na kiwanda cha misumali cha Vunjo.
Kutokana na malalamiko hayo, Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas Mawazo, alifanya ziara ya kushtukiza katika Kiwanda cha Fortune Paper na kuagiza kusimamishwa kwa shughuli zake kwa wiki moja baada ya kubainika kukiuka sheria za mazingira mara tatu licha ya kulipishwa faini.
Dkt. Nicas alieleza, kiwanda hicho kimepewa siku saba kufanya marekebisho ya mifumo yake ya mazingira, huku akisisitiza kuwa atarejea tena baada ya muda huo kujiridhisha kabla ya kuruhusu kuendelea kwa shughuli za uzalishaji.
Vilevile, aliitaka Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC )kwa kushirikiana na maofisa mazingira wa Manispaa ya Kibaha kufika katika viwanda ili kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wawekezaji na kutoa ufumbuzi wa haraka wa kudhibiti uchafuzi wa mazingira.
Hata hivyo, aliwaasa wawekezaji kuzingatia sheria za ujenzi sambamba na sheria za mazingira ili kuhakikisha shughuli zao haziathiri afya na ustawi wa wananchi wanaoishi karibu na viwanda hivyo.

Ofisa Mazingira wa Manispaa ya Kibaha, Rahel Ulaya, alisema mwekezaji wa Kiwanda cha Fortune Paper hajazingatia masharti ya mazingira, hivyo kwa mujibu wa agizo la Meya, shughuli za kiwanda hicho zimesimamishwa kwa muda hadi pale watakapojenga mifumo ya kisasa ya kuchuja maji taka ili kuzuia madhara kwa wananchi.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Mrisho Mlela, alifafanua ziara ya Meya huyo imebaini kuwepo kwa malalamiko makubwa ya uchafuzi wa mazingira yanayotokana na shughuli za viwanda, na kwamba tathmini ya kitaalamu imefanyika kutoa siku saba kwa kiwanda hicho kufanya marekebisho.
Mmoja wa wahusika wa uwekezaji wa kiwanda cha Fortune alikiri kupewa onyo mara kadhaa, na ameahidi kufanya marekebisho ambayo amepewa maelekezo ndani ya siku saba.




