Na Mwamvua Mwinyi, JamhueiMedia, Kibaha

BAADHI ya wakazi wa Mtaa wa Madafu, Kata ya Visiga, Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani, wameilalamikia Rasbery Farm, kiwanda cha kufuga kuku, kwa kusababisha kero ya nzi wengi na kuhofia kuhatarisha afya zao na kuathiri shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.

Wakazi hao akiwemo Sabra Selemani, Hassan Ngwanywama na Mzee Matimbwa, walitoa malalamiko yao kwa Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas Mawazo, wakati wa ziara yake ya kikazi katika kata hiyo.

Walisema nzi hao wamekuwa kero kubwa hususan nyakati za usiku, hali inayowaathiri wafanyabiashara na jamii kwa ujumla.

Sabra aliomba Kiwanda hicho kiangalie namna ya kuhifadhi taka mbichi zinazotokana na kinyesi cha kuku.

Mzee Matimbwa alisisitiza kuwa wawekezaji wanapaswa kufuata sheria na taratibu za mazingira ili kuepusha athari kwa wananchi wanaoishi jirani na viwanda.

Kwa upande wake, mkazi mwingine, Mzee Nonganonga, alilalamikia ujenzi holela katika baadhi ya maeneo ya kata hiyo na kuiomba Manispaa kupima na kupanga maeneo hayo ili kuepusha migogoro ya ardhi.

Akizungumza kuhusu kero hiyo, Mtendaji wa Kata ya Visiga, Aloisia Nyello, alisema ofisi yake imekwishapokea malalamiko hayo na wataalamu wa mazingira wamefanya tathmini na kubaini kuwa ni muhimu kupunguza idadi ya kuku kulingana na viwango vinavyotakiwa pamoja na kuongeza matumizi ya dawa za kuua nzi.

Kutokana na hali hiyo, Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas Mawazo, alitoa siku saba kwa uongozi wa Rasbery Farm kuhakikisha wanapuliza dawa maalum za kuua nzi hao ili kuondoa kero na hofu ya athari za kiafya kwa wananchi.

“Wananchi wamelalamika, viongozi tumefika kujionea na ni kweli. Tumetoa siku saba dawa zipulizwe ili kudhibiti nzi hawa na kulinda afya za wananchi,” alisema Dkt. Nicas.

Aidha, aliwaagiza maofisa afya na mazingira kuhakikisha wanafanya ukaguzi wa mara kwa mara katika viwanda na kwa wawekezaji ili kutoa maelekezo yanayozingatia sheria za mazingira.

Naye Msimamizi wa Rasbery Farm alikiri kuwepo kwa changamoto ya nzi, akisema kuwa kwa sasa wamekuwa wakipuliza madumu mawili ya dawa kila siku ili kupunguza tatizo hilo.

Aliahidi kuwa watatekeleza maelekezo ya Manispaa kikamilifu kabla ya muda wa siku saba uliotolewa.

Katika ziara hiyo, wananchi wa Kata ya Visiga pia waliwasilisha kero nyingine ikiwemo upatikanaji wa umeme, maji na barabara katika baadhi ya maeneo.