Na Mwandishi Wetu, Kiteto
Kishindo kimeanza tayari kwa mapokeo na utayari wa Wilaya ya Kiteto katika mpango wa Bima ya Afya kwa Wote kufuatia Kikao Maalum cha Kamati ya Afya ya Msingi (PHC) ngazi ya Wilaya kilichoketi Mjini Kibaya (Kiteto) tarehe 06 Januari,2026 kwa lengo la kutoa Elimu ya Awali na uelewa juu ya mpango huo wa Bima ya Afya kwa wote.
Mapema akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mhe. Remidius Mwema amesema kikao hicho ni hatua ya mwanzo ndani ya Wilaya kujenga uelewa wa kina juu ya mpango huo, kabla ya tarehe 08 Januari,2026 kuanza mfululizo wa Vikao maalum vya Tarafa zote saba (7) Wilayani humo na kuhakikisha makundi yote ndani ya Wilaya yanapata elimu ya awali juu ya mpango huo na kisha kufuatiwa na mikutano ya wananchi wote kwa kila Kijiji.
“Mpango wa Bima ya Afya kwa wote ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ndani ya siku 100 ikiwa ni dhamira njema ya kuimarisha huduma ya Afya kwa wananchi wote kupata bila kikwazo na tena kwa gharama nafuu” alibainisha Mhe. Mwema.
Aliongeza kuwa, Wilaya ya kiteto wamejipanga vema na kwamba kabla ya mpango huo kuzinduliwa rasmi na Mhe. Rais; jukumu la viongozi wa Wilaya hiyo ni kuwajengea uelewa na kutoa elimu kwa wananchi wote wa Wilaya ya Kiteto.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Kiteto Ndg. Mufandii Msaghaa amesema kuwa Mpango wa Bima ya Afya kwa wote haujaletwa kwa bahati mbaya, bali ni mpango wa Serikali kuhakikisha inatoa huduma kwa wananchi wake, na kuongeza kuwa wao viongozi wa Kiteto watahakikisha wananchi wanapata elimu sahihi.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto Mhe. Athumani Kilimo amesema hatua ya kuwajengea uelewa wananchi ni jambo muhimu sana, na kwamba wajumbe wote wa Kamati ya Afya ya Msingi katika Halmashauri ya Kiteto wanalo jukumu la kushusha Elimu hii kwa uwakilishi wa makundi na kuzingatia Jamii husika.
Pamoja na wajumbe wengine, kikao hicho pia kilihudhuriwa na Uwakilishi wa Viongozi wa Dini,Vyama vya Siasa, Makundi maalum,Viongozi wa Kimila ambao wote ni sehemu ya wajumbe halali wa kikao hicho.







