Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi wa matukio matatu ya vifo vilivyotokea kwa nyakati tofauti Tarime/Rorya, Jijini Arusha na Rufiji.
Tukio la kwanza ni la kifo cha Dickson Tadeus Joseph, mkazi wa Rebu Senta Wilayani Tarime kilichotokea tarehe 1.1.2025 huko katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime. Baada ya kutokea kifo hicho, Jeshi la Polisi limepokea barua ya malalamiko kuwa, kifo hicho hakikutokana na Dickson Tadeus Joseph (marehemu) kuanguka katika eneo la Mtaa wa Serengeti wakati akikimbia kama ilivyoelezwa awali bali kimesabababishwa na askari Polisi.
Uchunguzi wa kina umeanza na kulingana na ushahidi kutoka kwa watu walioshuhudia ikibainika kuna Askari aliyehusika hatua stahiki kwa mujibu wa sheria zitachukuliwa dhidi yake.
Tukio la pili ni la Viollete Uwumuhoza, Raia wa Rwanda ambaye alijinyonga tarehe 7.1.2026 akiwa mahabusu ya Polisi Jijini Arusha, alikokuwa akishiliwa kwa kosa la kuingia na kuishi nchini kinyume cha Sheria.
Uchunguzi wa kina ukihusisha uchunguzi wa kisayansi na wa haraka unaendelea kuhusiana na tukio hilo.
Sambamba na matukio hayo mawili, Jeshi la Polisi lina mshikilia askari mmoja wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji kwa tuhuma za kumpiga risasi Shaban Said Luluba, Mkazi wa Kijiji cha Nyamwage Wilayani Rufiji na kupelekea kupoteza maisha wakati akifanya ukamataji tarehe ya leo 8.1.2026.
Uchunguzi unaendelea na endepo itabainika kuna uzembe au matumizi zaidi ya nguvu hatua nyingine za kisheria zitachukuliwa dhidi ya askari huyo.


