Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia, Pwani

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha imemhukumu Stephano Anyosisye Mwasala (35), mkazi wa Msongola wilayani Kibaha, kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kuanzisha kituo cha kulelea watoto bila leseni, kubaka na kuwanyanyasa kingono watoto saba aliyokuwa anawalea.

Mwasala alikuwa mmiliki wa kituo cha kulelea watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu kiitwacho Majest Children Home, kilichopo Msongola, Kibaha.

Ilielezwa mahakamani kuwa, kwa nyakati tofauti kati ya Desemba 2024 na Januari 2025, mshtakiwa aliwaingilia kimwili na kuwafanyia vitendo vya kingono watoto hao saba wenye umri wa kuanzia miaka 10 hadi 14, waliokuwa chini ya uangalizi wake katika kituo hicho.

Upande wa Jamhuri uliieleza mahakama kuwa Jeshi la Polisi, kwa kushirikiana na Maafisa wa Ustawi wa Jamii, walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mara baada ya kupokea taarifa za tukio hilo, kisha upelelezi kufanyika na baadaye kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zilizokuwa zinamkabili.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mheshimiwa Joyce Mkhoi, alisema mshtakiwa amepatikana na hatia ya kuanzisha kituo cha kulelea watoto bila kuwa na leseni, kinyume na kifungu cha 146(2)(a) cha Sheria ya Mtoto, Sura ya 13 ya mwaka 2019, pamoja na makosa ya kubaka kinyume na vifungu vya 130(1), 130(2)(e) na 131(1) vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Marejeo ya mwaka 2022.

Mahakama ilimhukumu mshtakiwa kifungo cha maisha jela, ikieleza kuwa adhabu hiyo ni fundisho kwa watu wengine wanaokiuka sheria na kujihusisha na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na makundi mengine katika jamii.