Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Dar es Salam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deo Sangu, ametoa mwongozo rasmi kwa mawakala wote wanaowatafutia Watanzania ajira nje ya nchi. Hatua hii inalenga kuondoa mawakala wasio halali waliokuwa wakisababisha matatizo kwa wananchi.
Ameyasema hayo Januari 9, 2026, jijini Dar es Salaam, katika hafla ya kuwaaga Watanzania wanaoenda kufanya kazi katika nchi mbalimbali.
Waziri Sangu amebainisha kuwa mawakala wote waliokuwa wakijihusisha na shughuli zisizo halali wametimuliwa na leseni zao kuondolewa. Serikali itashirikiana na mawakala waliokidhi vigezo vya kisheria ili kuhakikisha usalama wa Watanzania wanaoenda kufanya kazi nje ya nchi.

Katibu Mkuu wa wizara, Bi. Zuhura Yunus, amesema serikali inaendelea kuboresha mazingira wezeshi kwa vijana kupata ajira nje ya nchi. Hatua hizi ni sehemu ya mkakati wa kupunguza ukosefu wa ajira, kuongeza kipato, na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Bi. Yunus ameongeza kuwa ushirikiano na nchi zinazopokea wafanyakazi pamoja na mawakala binafsi waliothibitishwa utaimarisha usalama wa kisheria, mazingira salama ya kazi, na heshima ya haki za wafanyakazi.
Maonesho ya Ajira kwa Vijana
Wizara imepanga kuandaa maonesho ya kazi yanayojumuisha mawakala na wadau mbalimbali. Lengo ni kuwafahamisha vijana kuhusu fursa sahihi za ajira nje ya nchi na kupunguza hatari za ushirikiano na mawakala wasio halali.

Serikali inasisitiza kuwa hatua hizi ni endelevu na zimekusudiwa kuhakikisha fursa za ajira nje ya nchi zinapatikana kwa usalama, uwazi, na kwa manufaa ya taifa.
Naye Mwakilishi kutoka NSSF Lulu Mengele amewasisitiza Vijana hao kujiunga na mfuko wa hifadhi Jamii Kwa kujiwekea akiba Kupitia mshahara watakaoenda kulipwa ili wanaporudi wasiwe na shaka na Maisha yao






