๐ Bariadi- Simiyu
Serikali imewataka wakandarasi wazawa wanaotekeleza miradi ya Umwagiliaji nchini kuhakikisha miradi hiyo inaleta tija kwa wakulima na taifa kwa ujumla, ikisisitiza kuwa uzembe au kuchelewesha utekelezaji kutaibua hatua kali za kisheria dhidi yao.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) akiwa katika muendelezo wa ziara yake mkoani Simiyu, wakati wa kukagua maendeleo ya ujenzi wa Bwawa la Umwagiliaji la Kasoli lililopo Kijiji cha Kasoli, Kata ya Kasoli. Bwawa hilo lina ujazo wa takribani mita za ujazo milioni 2.7 na linatarajiwa kuhudumia mashamba yenye ukubwa wa hekta 650.

Mhe. Silinde amesema kuwa uamuzi wa Serikali kuwapa wakandarasi wazawa miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo ya Umwagiliaji, unalenga kuwajengea uwezo na kukuza ujuzi wa ndani ili wazawa washiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa nchi yao. Amesisitiza kuwa imani hiyo lazima iendane na uwajibikaji, ubora wa kazi na kukamilisha miradi kwa wakati uliopangwa.
โSerikali inawapa nafasi wakandarasi wazawa kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuimarisha uchumi wa ndani. Hata hivyo, ni wajibu wao kuhakikisha miradi hii inaleta matokeo chanya kwa wakulima, kinyume chake hatua zitachukuliwa” amesema Mhe. Silinde.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe..Anamringi Macha, amepongeza juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Kilimo katika kuwawezesha wakulima kuondokana na kilimo cha kutegemea mvua, akibainisha kuwa mradi wa Bwawa la Kasoli ni miongoni mwa uwekezaji mkubwa uliofanywa ndani ya Mkoa wa Simiyu.

โHili ni kati ya mabwawa makubwa yenye uwekezaji mkubwa katika Wilaya yetu ya Bariadi na hata Mkoa wetu wa Simiyu kwa ujumla, ni nitegemeo kubwa kwa maendeleo ya kilimo cha Umwagiliaji” amesema Mhe. Macha.
Ujenzi wa Bwawa la Kasoli umefikia asilimia 90.2 na kukamilika kwake kunatarajiwa kunufaisha zaidi ya wakulima 15,000, hususani wanaojishughulisha na uzalishaji wa mazao ya mpunga, mahindi na mbogamboga, hivyo kuongeza tija ya uzalishaji, kipato cha wakulima na usalama wa chakula katika Mkoa wa Simiyu na maeneo jirani.







