




Na Antonia Mbwambo – Manyara
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray amewataka watumishi wa Umma kutambua wajibu wao katika kutekeleza majukumu ya kila siku ili kufanya kazi kwa uwezo, maarifa na ujuzi walio nao kwa lengo la kuboresha huduma ikiwa ni mojawapo ya njia ya kuwatumikia wananchi kwa ustawi wa Taifa.
Mhe. Qwaray ameyasema hayo tarehe 8 Januari, 2026 Mkoani Manyara wakati akizungumza na watumishi wa umma ngazi ya Mkoa, Halmashauri ya Mji wa Babati na Hamashauri ya Wilaya ya Babati wakati alipokuwa katika ziara yake ya kikazi ambapo ni ziara ya kwanza Mkoani hapo tangu alipoteuliwa tarehe 17 Novemba, 2025 na Mhe Raisi wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Amesema Waajiri wote wa Taasisi za Umma lazima waweke kipaumbele katika kushugulikia changamoto zinazowakumba watumishi waliopo chini yao ikiwemo madai ya kupandishwa vyeo na malimbikizo ya mishahara ili kuongeza dhana ya uwajibikaji na kupunguza malalamiko ya watumishi hao.
“Ukiona mtumishi wa umma anakuja hadi Wizarani kwa ajili ya kufuatilia utatuzi wa changamoto zake za kiutumishi, ujue wewe kama msimamizi hujawajibika ipasavyo”,Mhe. Qwaray alisema.
Pia Mhe. Qwaray amewataka watumishi kuzingatia Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma ambazo zinaelekeza tabia na mienendo ambayo mtumishi anapaswa kuwa nayo anapokuwa anatoa huduma katika eneo lake la kazi.
“Mtumishi anapokuwa eneo la kazi hana budi kuachana na masuala binafsi na kujikita katika utoaji wa huduma kwa mwananchi ili kutumia vizuri rasilimali za Serikali katika kuhakikisha kila anayefika kupata huduma anaipata kwa wakati”, Mhe. Qwaray alisema.
Aidha amesisitiza matumizi ya mifumo iliyopo na inayotumika katika kushughulikia masuala mbalimbali ya kiutumishi ikiwemo maombi ya uhamisho na likizo ili kuendana na teknolojia iliyopo kwa lengo la kuwa na utendaji unaozingatia muda na usawa.
Mhe. Qwaray alihitimisha kwa kutoa wito kwa watumishi wa umma kuwa wazalendo na wenye kutanguliza Maslahi ya Taifa mbele katika kulinda na kuimarisha Amani ya nchi kwa kutoa huduma bora, kuzingatia maadili ya kazi na kuepuka vitendo vinavyoweza kuleta mgawanyiko katika jamii.

