Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Simiyu
NAIBU Waziri wa Kilimo David Silinde (Mb), ameeleza kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa miradi mitatu mikubwa ya umwagiliaji ikiwemo ujenzi wa Bwawa la Nyida lililopo mkoani Shinyanga, Kasoli Bariadi mkoani Simiyu na Bugwema mkoani Mara.
Waziri Silinde amesema hayo katika muendelezo wa ziara yake mikoani humo na kusisitiza kuwa maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo inaendana na thamani ya uwekezaji unaofanywa na Serikali hivyo wananchi ni vyema kuitunza miradi hiyo muhimu katika maendeleo ya sekta ya Kilimo.

Amesema ameridhishwa na hatua iliyopo ujenzi wa Bwawa la Nyida na mara baada ya ujenzi huo kukamilika wananchi watapata fursa mpya ya kuimarisha kilimo kupitia mradi wa Umwagiliaji, mradi unaotarajiwa kuongeza uzalishaji wa mazao, hususan mpunga na kuboresha maisha ya kaya zaidi ya 1,500.
Amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kumkomboa mkulima kutoka kilimo cha kutegemea mvua na kuhimiza kilimo cha uhakika kupitia Umwagiliaji.
Naibu Silinde alisema Tume chini ya Wizara ya Kilimo itakamilisha asilimia 10 iliyobaki ya ujenzi wa mradi na kuongeza eneo la Umwagiliaji kutoka hekta 425 hadi kufikia zaidi ya hekta 800 ambapo usanifu wa eneo lililoongezeka umeanza.

Ametumia fursa hiyo kuwaasa wakulima kulipa Ada ya huduma za umwagiliaji ili kuunga mkono jitihada za Serikali.
Akiwasilisha taarifa ya mradi, Mhandisi wa Umwagiliaji Shinyanga Ebenezer Kombe amesema bwawa la Umwagiliaji Nyida lina uwezo wa kuhifadhi lita bilioni 7.8 za maji, likihudumia hekta 800 za mashamba na kuongeza eneo la umwagiliaji hadi hekta 1,500 katika maeneo jirani.
Aidha katika msimu huu wa Kilimo wananchi wameanza kunufaika na mradi huo kwa kuanza kutumia maji ya Bwawa kwa ajili ya Umwagiliaji na kuanza kuvuna samaki ambapo bwawa hilo pia litakuwa likitumika kwa ajili ya ufugaji wa samaki na eneo la mabirika ya kunyweshea mifugo.

“Mradi unatekelezwa na Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2025/2026, Mkoa umepanga kulima hekta 661,236 za mazao ya chakula na hekta 99,814 za mazao ya biashara, huku Umwagiliaji ukiwa nguzo muhimu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,”amesema.
Mradi wa Bwawa la Nyida umeanza ujenzi January mwaka 2023 na unatarajiwa kukamilika Mei 2026 hadi sasa umefikia zaidi ya asilimia 90.
Akiwa katika Bwawa la Kasoli Naibu Waziri Silinde ameeleza kuridhishwa na hatua za ujenzi zilizopo katika mradi huo uliopo wilaya ya Bariadi mkoa wa Simiyu.
Aidha ujenzi huo umeanza mnamo tarehe 16/01/2023 na utakamilika tarehe 05/05/2026 ambapo umefikia asilimia 90.2 na mradi uko kwenye hatua ya mwisho kukamilika.

Amesema bwawa hilo lina ujazo wa takribani mita za ujazo milioni 2.7 na linatarajiwa kuhudumia mashamba yenye ukubwa wa hekta 650, ambapo mradi wa ujenzi wa mifereji utanza baada ya mkandarasi kupatikana.
Naibu Waziri Silinde pia amewahakikishia wananchi wa Mara kuwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea na hatua za ujenzi wa miundombinu ya Umwagiliaji katika Shamba la Bugwema na lengo la Serikali ni kuhakikisha ujenzi huo unawanufaisha wakulima kwa kuwa na Umwagiliaji eneo jumla ya hekta 3000.
“Mradi huu tayari Mkandarasi aneshasaini mkataba na atakabidhiwa ili kuanza ujenzi mwezi ujao na kazi zitakazo fanyika ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya Umwagiliaji ambapo wakulima zaidi ya 3000 watanufaika,”amesema.


