Baada ya Tanzania kupiga hatua kubwa katika kudhibiti na kukomesha biashara na matumizi ya dawa za kulevya, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema nchi sasa inakabiliwa na changamoto mpya ya kuongezeka kwa ulevi wa pombe, hususan miongoni mwa vijana.
Akizungumza Januari 9, 2026 katika kikao kazi kati ya DCEA na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kamishina Jenerali wa Mamlaka hiyo, Aretas Lyimo, amesema mafanikio yaliyopatikana yamepunguza kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa dawa za kulevya mitaani, hali iliyosababisha baadhi ya waliokuwa waraibu kuelekeza nguvu zao katika matumizi ya pombe kupita kiasi.
Lyimo amesema kwa sasa dawa hatarishi kama heroin na cocaine hazipatikani kirahisi kama ilivyokuwa awali, jambo lililotokana na ushirikiano wa karibu kati ya DCEA, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi.

Ameeleza kuwa hali hiyo imeifanya Tanzania kuondokana na taswira ya kuwa njia ya kupitisha dawa za kulevya kwenda nchi nyingine, huku akibainisha kuwa hata ukaguzi mkali uliokuwa ukifanywa kwa wasafiri wa Kitanzania katika viwanja vya ndege vya nje ya nchi umepungua kutokana na mafanikio hayo.
Hata hivyo, Lyimo amesema pengo lililoachwa na kukosekana kwa dawa za kulevya sasa limezua changamoto ya kijamii, ambapo vijana wengi wameingia kwenye matumizi ya pombe kupita kiasi, hali inayohitaji mkakati mpya wa kitaifa.
Amesema DCEA ina jumla ya soba 78 nchini, ambazo kwa kiwango kikubwa zimejaa waraibu wa pombe, hali inayoonesha ukubwa wa tatizo hilo linalohitaji nguvu mpya za pamoja kulikabili.
Kamishina Jenerali huyo amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mapambano dhidi ya ulevi wa pombe sambamba na kuhamasisha waraibu kujiunga na soba ili kupata tiba na kurejea katika maisha yenye tija.

Akizungumzia kikao kazi hicho, Lyimo amesema vyombo vya habari ni wadau muhimu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya na ulevi kwa ujumla, akibainisha kuwa elimu kwa umma kupitia habari na makala ni nyenzomuhimu ya kuzuia tatizo hilo kuendelea kukua.
Ameongeza kuwa kikao hicho kimeandaliwa kwa lengo la kubadilishana uzoefu, kujengana uwezo na kuweka mikakti mipya itakayosaidia kukabiliana na changamoto zinazojitokeza baada ya mafanikio dhidi ya dawa za kulevya.



