*Upatikanaji wa Nishati Safi ya Kupikia waongezeka zaidi ya mara tatu ndani ya kipindi cha miaka minne pekee

*Yasema ipo tayari kushirikiana na Taasisi za Kimataifa zinazotoa ufadhili kwa nia ya kupunguza matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia hasa barani Afrika

*Yatumia Jukwaa la Kimataifa la IRENA lenye wanachama 171 kueleza fursa za uwekezaji katika Nishati Safi ya Kupikia

ABU DHABI, UAE

Imeelezwa kuwa, Tanzania inaendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata nishati safi, salama na nafuu ya kupikia, kwa kuhakikisha fedha za kuwezesha miradi ya nishati safi ya kupikia zinapatikana kutoka Serikalini, Sekta Binafsi, Wadau na Mashirika ya Kimataifa yanayounga mkono jitihada za matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia duniani.

Akizungumza katika Mkutano wa pembeni wa Baraza la Kimataifa Nishati Jadidifu (IRENA), uliohusu suala la upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya Nishati Safi ya Kupikia, Abu Dhabi katika Falme za Kiarabu, Mhandisi Anita Ringia kutoka Wizara ya Nishati, amesema Tanzania imeendeelea kutenga na kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia na matokeo yake yanaonekana kupitia upatikanaji wa nishati safi ya kupikia.

Amesema.upatikanaji wa Nishati Safi ya Kupikia umeongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 23.2 mwaka 2025, ikiwa ni zaidi ya mara tatu ndani ya kipindi cha miaka minne pekee.

Amesema mafanikio hayo yametokana na uongozi thabiti wa Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameifanya nishati safi ya kupikia kuwa kipaumbele cha kitaifa na nguzo muhimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Katika hatua nyingine, Ringia amesema Tanzania katika mwaka wa fedha 2025/26 inaendelea na miradi mbalimbali ikiwemo usambazaji wa majiko banifu 200,000 yenye ruzuku, kulipia majiko ya umeme 480 kupitia bili ya umeme kwa kushirikiana na TANESCO katika mradi wa majaribio, na kusambaza mitungi zaidi ya 450,000 ya gesi ya LPG kwa bei ya ruzuku.

Ameongeza kuwa Serikali pia imepiga marufuku matumizi ya kuni na mkaa katika taasisi zinazohudumia zaidi ya watu 100 kwa siku, hatua iliyolenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi katika zaidi ya taasisi za umma 31,000 uwekezaji unaohitaji zaidi ya bilioni 1 za kimarekani, sambamba na kuimarisha kampeni za uhamasishaji na kusaidia biashara ndogo na za kati katika sekta hiyo.

Mhandisi Ringia amebainisha kuwa mafanikio hayo yameungwa mkono pia Sekta binafsi nchini kupitia ongezeko la uwekezaji wa taasisi za kifedha za ndani, zikiwemo Benki ya NMB na CRDB, ambazo zimeanza kutoa mikopo kwa riba nafuu kwa wajasiriamali wa nishati safi ya kupikia ili kupanua mitandao ya usambazaji nchi nzima.

Katika Mkutano huo, Mhandisi Ringia ametangaza fursa mbalimbali za uwekezaji katika ujenzi wa miundombinu ya kupokea, kuhifadhi na kusambaza nishati safi ya kupikia, ujenzi wa viwanda vya ndani vya kutengeneza majiko, vifaa, na mitungi na uwepo wa fursa bunifu za kuwezesha wananchi kulipia nishati kupitia mifumo ya kulipia kidogo kidogo (PAYGO), kulipia kwa riba nafuu na kulipia kupitia bili za umeme.

Akizungumza kuhusu suala la mchango wa kimataifa katika kuwezesha fedha za kutekeleza Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia, Mhandisi Anita amesema Tanzania inaunga mkono wito wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi za kifedha, na washirika wa maendeleo ili kuziba pengo la ufadhili wa nishati safi ya kupikia, hususan barani Afrika ambako karibu watu bilioni moja bado hawana huduma hiyo.

Wataalam wengine wakiongozwa na Kamishna Msaidizi anayeshughulikia Nishati Jadidifu, Imani Mruma walishiriki vikao vya awali vilivyohusu masuala ya utungaji wa sheria, udhibiti, uandaaji wa mipango na uwekezaji wa miradi ya Nishati Jadidifu.

Katika vikao hivyo Tanzania ilieleza kuhusu juhudi inazochukua katika kuhakikisha Nishati Jadidifu inakuwa na mchango wa kutosha katika gridi ya Taifa ili kuendana na maendeleo endelevu ya matumizi ya nishati jadidifu duniani (SDG 7) .

Katika Nishati Jadidifu Tanzania imeeleza kuwa inazidi kupiga hatua ambapo mchango wake unaoingizwa kwenye gridi ya taifa ni asilimia 68 huku juhudi nyingine zikiendelea.ikiwemo ya ujenzi wa mradi wa umeme Jua wa Kishapu wa MW 150 ambao ifikapo Februari mwaka huu utakuwa umeanza kuzalisha umeme kiasi cha MW 50.

Aidha vyanzo vingine vya Nishati Jadidifu vinavyoendelezwa ni pamoja na vyanzo vya Jotoardhi katika ziwa Ngozi (70MW) Songwe (5MW) kiejombaka (60MW), Natron (60MW) na Luhoi (5MW).

Akifungua Mkutano wa IRENA katika siku yake ya kwanza, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IRENA, Gaun Singh amehimiza kila nchi wanachama kuzidi kuwekeza kwenye miradi ya nishati jadidifu ambapo lengo la kidunia ni kuwa na umeme wa GW 11,000 zinazotokana na nishati jadidifu ifikapo 2030.

Mkutano wa IRENA 2026 unaongozwa na kaulimbiu ya “Matumizi ya Nishati Jadidifu kwa manufaa ya pamoja kwa kila binadamu” yaani “Powering Humanity: Renewable Energy for Shared Prosperity”.