Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mwanza

Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, inaendea kuinua hadhi ya Mkoa wa Mwanza, kupitia utekelezaji wa Miradi ya Umwagiliaji kutokana na wananchi kuanza kunufaika na ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Mahiga.

Mradi huo umetajwa kuwa umeleta mapinduzi makubwa katika shughuli za kilimo.Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Davidi Silinde, mkoani humo.

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa miradi 12 ya Umwagiliaji inayotekelezwa mkoani humo, ambapo minne inafanya kazi kikamilifu na mingine minane ipo katika hatua za ukarabati.

Mheshimiwa Silinde amesema kuwa mabonde 43 yameainishwa kuwa na uwezo wa kilimo cha Umwagiliaji na kwamba miradi mitatu ya sekta binafsi imeonesha mchango wa wadau katika kuendeleza sekta hii muhimu.

“Kiufupi niseme kwamba nimezungukia miradi mingi lakini mradi wa Mahiga uliopo Wilayani Kwimba umefanya vizuri zaidi,”amesema.

Ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo unatokana na maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amesisitiza wakulima waache kutegemea kilimo cha msimu kinachotegemea mvua pekee na badala yake kujikita katika kilimo cha Umwagiliaji.

Kwa mujibu wa Mhe. Silinde, miradi ya ukarabati imekuwa chachu ya mageuzi makubwa ambapo Skimu ya Katunguru yenye hekari 3,750 imefikia asilimia 90 ya utekelezaji na inatarajiwa kukamilika Mei 2026.

Ameongeza kuwa mbali na mradi huo pia Skimu ya Sukuma inayohudumia hekari 500 tayari imekamilika na kukabidhiwa kwa wakulima, huku Mahiga ikihudumia hekari 1,000 ikikamilika Januari 2026.

Kwa mujibu wa Silinde, skimu ya Magurukenda pia inayohudumia hekari 500 imeshakabidhiwa kwa chama cha Umwagiliaji.

Waziri Silinde amesema kuwa jumla ya gharama za ukarabati wa miradi hiyo ni zaidi ya shilingi bilioni 13.4, na inatarajiwa kunufaisha zaidi ya wakulima 4,000.

Aidha ameongeza kuwa mbali na ukarabati, mabonde 19 yapo katika hatua za usanifu wa kina na upembuzi yakinifu, yakihusisha wilaya za Kwimba, Magu, Ukerewe, Sengerema/Buchosa na Misungwi.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri, utekelezaji wa miradi hiyo ni ushahidi wa mipango ya muda mrefu ya kuhakikisha kilimo cha Umwagiliaji kinapanuka na kuleta tija kwa wakulima wadogo na wakubwa.

Vilevile amebainisha kuwa mpango wa uchimbaji wa visima vitano kwa kila halmashauri umeanza, na vifaa vya kisasa kama pampu na betri tayari vimewasili mkoani Mwanza, hatua inayotarajiwa kuongeza upatikanaji wa maji kwa kilimo na matumizi ya kijamii.

Mhe. Silinde amesisitiza kuwa manufaa ya miradi hiyo ni makubwa na ya moja kwa moja kwa jamii, kwani kupitia kilimo cha Umwagiliaji, wakulima wanapata uhakika wa kilimo, uwezo wa kulima mara mbili kwa mwaka na kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.

Kwa mujibu wa Silinde, Umwagiliaji unachochea kilimo cha kibiashara, kuongeza kipato cha kaya, mapato ya halmashauri na mkoa na hatimaye kuchangia pato la Taifa.

Akihitimisha, Naibu Waziri huyo wa Kilimo alisema kuwa utekelezaji wa miradi ya Umwagiliaji Mwanza ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya kuondoa utegemezi wa mvua, kuongeza tija na kuimarisha usalama wa chakuli

“Miradi hii ni dira ya jinsi kilimo kinavyoweza kubadilisha maisha ya wananchi na kuchangia ajenda ya maendeleo ya kitaifa,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Mhe. Ng’walabuza Ludigija ameipongeza Wizara ya Kilimo kwa juhudi kubwa inazozifanya kuhakikisha wakulima wanapata fursa ya kulima kwa tija, kuongeza uzalishaji na kuinua uchumi wao pamoja na upatikanaji wa chakula cha kutosha.

Naye Mhandisi wa Umwagiliaji wa Mkoa wa Mwanza amesema mradi wa skimu ya Umwagiliaji ya Mahiga unatekelezwa kwa viwango vya juu vya kitaalamu, ukiwa umejumuisha ujenzi wa miundombinu muhimu ikiwemo mifereji mikuu miwili yenye urefu wa jumla ya mita 5,500, mifereji ya shambani, barabara za mashambani zenye urefu wa mita 5,000, vigawa maji, birika la kunyweshea mifugo na kuongeza kimo cha tuta la bwawa, yote yakilenga kuhakikisha maji yanawafikia wakulima kwa ufanisi na kuongeza uzalishaji wa mazao.