Kufuatia habari iliyoiripotiwa kupitia ukurasa wa Instagram wa Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, tarehe 11 Januari, 2026 kuhusu tukio la ukatili dhidi ya mtoto katika eneo la Kinyerezi, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limethibitisha kumkamata mtuhumiwa wa tukio hilo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, mtuhumiwa huyo ni Joseph Daudi Mwakalinga, mkazi wa Zimbili, Kinyerezi, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam.

Taarifa ya Polisi inaeleza kuwa mtuhumiwa anadaiwa kumjeruhi mtoto wake (jina limehifadhiwa) kwa kumpiga kwa fimbo na kumchoma moto, tukio linalodaiwa kutokea Januari 08, 2026 katika eneo la Kinyerezi. Polisi wamesema mtuhumiwa huyo anashikiliwa kwa mahojiano zaidi huku taratibu za kisheria zikiendelea.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema hatua zaidi zinaendelea kuchukuliwa kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za kisheria, na limetoa wito kwa wazazi, walezi na wananchi kwa ujumla kujiepusha na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na kuendelea kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama pindi wanapobaini matukio ya ukiukwaji wa haki za mtoto.

Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima, amelipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua za haraka zilizochukuliwa dhidi ya mtuhumiwa, sambamba na kuwapongeza wananchi na wadau wote waliotoa taarifa na kupaza sauti zilizowezesha hatua hizo kuchukuliwa. Waziri Gwajima ameitaka jamii kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa mamlaka husika kwa kutoa taarifa za vitendo vya ukatili mara vinapotokea ili vitendo hivyo vitokomezwe kabisa. Aidha, ameahidi kupitia wizara yake kupokea kila taarifa na kuifuatilia kikamilifu hadi hatua ya mwisho ya haki.