Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka Majaji na Mahakimu nchini kusimamia haki kwa kuzingatia sheria, maadili na viapo vyao ili kulinda amani, usalama na utulivu wa Taifa.

Rais Samia ametoa wito huo jana jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Mahakimu na Majaji, akisisitiza kuwa Mhimili wa Mahakama una nafasi muhimu katika ujenzi wa Taifa lenye haki, amani na utawala bora.

Alisema kuwa ni wajibu wa watoa haki kusimama kwenye mstari wa haki wanapotoa maamuzi bila hofu, huba wala upendeleo, kama walivyoapa wanapoingia katika utumishi wa Mahakama.

“Ningependa sana msimamie kiapo chenu mnapoapa kusimamia haki kwa kuzingatia sheria na maadili bila hofu, upendeleo, huba wala chuki,hiki ndicho kiapo chenu, na ningependa mkisimamie kwa vitendo,” alisema Rais Samia.

Aliongeza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025/2050 imejengwa juu ya misingi ya utawala bora, amani, usalama na utulivu, akieleza kuwa mafanikio ya dira hiyo hayawezekani bila kuwa na Mahakama imara, huru na inayoaminika na wananchi.

“Dira ya 2050 inatambua kuwa utawala wa sheria ni msingi wa maendeleo endelevu,Serikali imechukua na itaendelea kuchukua hatua za kuijenga Mahakama iwe imara na inayotoa haki kwa wananchi,” alisema.

Akizungumzia changamoto za maslahi ya watumishi wa Mahakama, Rais Samia aliwataka Majaji na Mahakimu kuwa wavumilivu, akibainisha kuwa watumishi wa sekta nyingine pia wanakabiliwa na changamoto kubwa.

“Nikisema hivyo haimaanishi kuwa Serikali haitashughulikia maslahi yenu,maendeleo ni hatua, na tumeanza kuchukua hatua kubwa za kurejesha heshima ya Mahakama yetu,safari ni ya polepole lakini inaendelea,” alisisitiza.

Aidha, Rais Samia alisema Watanzania wana matumaini makubwa na Mahakama, wakitarajia kuona haki, uwazi, misingi ya kikatiba na utu vikizingatiwa katika utoaji wa maamuzi, akionya dhidi ya vitendo vya kubambikiza wananchi kesi vinavyonyima watu uhuru wao bila haki.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, George Masaju, aliwasilisha mapendekezo ya Chama cha Mahakimu na Majaji, yakiwemo kuboreshwa kwa maslahi ya watumishi wa Mahakama na kuhamishiwa kwa mashauri yote ya migogoro ya ardhi kusikilizwa na Mahakama kuanzia ngazi ya mwanzo hadi ngazi za juu, badala ya mabaraza ya kata na ardhi.

Alisema Mahakama ipo tayari kushirikiana na Wizara husika pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuandaa rasimu ya muswada wa marekebisho ya sheria ili kuwezesha utekelezaji wa mabadiliko hayo kwa lengo la kuondoa mkanganyiko na kuimarisha utoaji wa haki katika migogoro ya ardhi.