Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Katika siku za karibuni, sauti za vijana waliotaka kuandamana zilisikika kwa nguvu katika mitaa na kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii.

Sauti hizi, bila kujali mtu anazipokea kwa hisia zipi, zina ujumbe mmoja muhimu: kuna sehemu ya jamii inayohisi kusikilizwa hakutoshi. Hilo si jambo la kupuuzwa wala la kubezwa. Ni ishara ya kizazi kinachotafuta nafasi yake, haki yake na mustakabali wake katika taifa.

Sitanii, niseme mapema tu kuwa nakubaliana na vijana au kundi lolote katika jamii kudai haki ya aina yoyote inayoweza kuboresha maisha yao kutoka walipo na kusonga mbele.

Nisichokubaliana nacho ni matumizi ya nguvu katika kudai haki. Kila nchi ina utamaduni wake, zipo nchi kama majirani zetu hapa Kenya wao uhuru walipata kwa mapigano ya Mzungu Arudi Ulaya, Mwafrika Apate Uhuru (MAUMAU). Sisi Tanzania tulipata uhuru kwa njia ya mazungumzo. Ni kwa msingi huo tusisahau methali kuwa “Nguo ya kuazima haistili…”

Ni ukweli usiopingika kwamba Tanzania imejijengea historia ya amani, utulivu na maridhiano. Amani hii haikuja kwa bahati mbaya; ilijengwa kwa hekima ya viongozi, uvumilivu wa wananchi na utamaduni wa kusikilizana hata pale tofauti zinapokuwa kubwa. Ndiyo maana, katika nyakati kama hizi, busara hutulazimu zaidi kuliko jazba.

Serikali, kama chombo kikuu cha kusimamia masilahi ya umma, ina wajibu wa kisheria na kimaadili wa kusikiliza kilio cha wananchi wake, hususan vijana ambao ndio wengi na ndio nguvukazi ya taifa. Kusikiliza hakumaanishi kukubaliana na kila dai, bali ni kufungua milango ya mazungumzo ya wazi, ya heshima na yenye lengo la kutafuta suluhu za kudumu. Maridhiano huanza pale pande zote zinapokubali kwamba hakuna mwenye haki ya kudharau mwenzake.

Stanii, kwa upande wao, vijana wanapaswa kutambua kwamba madai yenye mashiko yanahitaji njia zenye busara. Historia ya dunia inaonyesha kuwa mataifa yaliyofanikiwa si yale yaliyosukumwa na hasira pekee, bali yale yaliyotumia mazungumzo, hoja na mipango thabiti kushinikiza mabadiliko. Kuandamana kunaweza kuwa haki ya kidemokrasia, lakini si haki inayopaswa kutumiwa bila kuzingatia usalama wa watu, mali zao na amani ya taifa.

Hadi leo tunaona majengo, magari, vituo vya mafuta na pikipiki zilizochomwa moto maeneo mbalimbali nchini. Hii haikuwa bahati mbaya, ilipangwa. Maisha ya watu yamepotea. Wapo wanaoifurahia hali hii, wanaona inawasogeza karibu na kwenda Ikulu.

Zinasikika sauti za kumwita Mzungu atuongoze eti katika kipindi cha mpito. Kwa kweli bila kupepesa macho, mkoloni alikwisha kuondolewa. Tujadili jinsi ya kuleta maendeleo kwa taifa letu, ila si kwa njia ya kumrejesha mkoloni kutuundia serikali.

Jamii nayo ina nafasi muhimu katika mchakato huu. Wazazi, viongozi wa dini, wanazuoni, wanahabari na wadau wa maendeleo wanapaswa kuwa madaraja, si kuta. Wanapaswa kusaidia kutafsiri madai ya vijana kwa lugha inayojenga, na wakati huohuo kuisaidia serikali kuyaona madai hayo kama fursa ya kujirekebisha, si tishio. Taifa linapokosa madaraja ya mawasiliano, ufa mdogo hubadilika kuwa shimo kubwa.

Sitanii, ni wakati wa kuimarisha majukwaa ya mazungumzo ya kitaifa yanayojumuisha vijana, serikali na sekta binafsi. Majukwaa haya yawe si ya dharura tu, bali ya kudumu, ili kero zisikusanyike hadi kulipuka. Serikali imetangaza ajira zaidi ya 41,000, hizi ziendelee kusemwa hadi ziingie masikioni mwa watu. Tusiseme wataziona tu. Gharama za maisha, ushiriki wa vijana katika uamuzi, na haki za msingi ni mada zinazohitaji mikakati ya vitendo, si ahadi tupu.

Maridhiano ya kweli yanahitaji ujasiri wa kweli inapokuwa mambo hayakwenda sawa, na dhamira ya pamoja ya kurekebisha. Serikali inapopiga hatua ya kusikiliza na jamii inapochagua busara badala ya mihemko, taifa hushinda. Tanzania imewahi kuvuka mawimbi makubwa kwa maridhiano; haina sababu ya kushindwa sasa.

Tunakumbuka wimbi la Zanzibar mwaka 2001. Tulilimaliza wenyewe baada ya kuwashinda wasuluhishi wa kimataifa akina Chifu Emeka Anyaoku aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola. Alijaribu kusuluhisha akashindwa. Mwaka 2010 Maalim Seif Sharif Hamad akakaa na Rais (mstaafu) Amani Abeid Karume, wakalimaliza tatizo la Zanzibar kimyakimya.

Leo Zanzibar ni shwari kuliko wakati wowote. Hili lililotokea limo ndani ya uwezo wetu. Jumuiya ya Madola ilipata kushindwa kutatua mgogoro wa Zanzibar tukautatua wenyewe. Hata hili uwezo tunao.

Mwisho, vijana si tatizo; ni jibu. Serikali si adui; ni chombo cha wananchi. Jamii si mtazamaji; ni mshiriki. Tukikubali ukweli huo, tutatambua kwamba kujenga maridhiano na kufanyia kazi madai ya vijana si ishara ya udhaifu, bali ni alama ya ukomavu wa taifa linalojitambua na kuthamini amani yake.

Vyama vya siasa; CCM, CHADEMA, ACT-Wazalendo na vingine, vinayo nafasi ya kuliinua taifa letu kwa mazungumzo, kwa kuweka kando jazba. Serikali imeanza kwa kuunda Wizara ya Vijana inayoongozwa na kijana mwenzao, Dk. Joel Nanauka.

Rais Samia Suluhu Hassan ameishatamka hadharani kuwa yuko tayari kunyoosha mkono. Tume ya Uchunguzi imeundwa kutafuta ukweli wa kilichotokea Oktoba 29, 2025. Ndani ya serikali ninazo taarifa kuwa wengi wameanza kuwajibishwa hata kabla ya matokeo ya uchunguzi. Mmoja wa mawaziri wa zamani anashikiliwa na mengine mengi. Mimi ninaamini sisi Watanzania tunao uwezo wa kutoka hapa tulipo salama kwa njia ya mazungumzo. Tuchague njia hii. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404 827