Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani,
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Shangwe Twamala, amewataka Madiwani wa Halmashauri za Wilaya ya Kibaha na Chalinze kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma, ikiwemo mapato na fedha za Serikali na kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa kuzingatia thamani ya fedha .
Akizungumza Januari 16, 2026, wakati wa kuhitimisha mafunzo elekezi ya kuwajengea uwezo madiwani hao, Twamala amesema mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha madiwani kutekeleza majukumu ili kuleta matokeo chanya kwa wananchi.
Amesisitiza Serikali inatarajia kuona mabadiliko yatokanayo na maarifa na ujuzi walioupata kupitia mafunzo hayo.

Twamala ameeleza ,madiwani wanapaswa kuzingatia misingi ya utawala bora, kuheshimu sheria, kanuni na taratibu na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali, hususan katika kuboresha huduma za kijamii na kuchochea ukuaji wa uchumi .
Aidha amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya madiwani, wataalamu na wananchi, sambamba na kuepuka migogoro isiyo ya lazima inayoweza kukwamisha maendeleo.
Nae Hassani Mwinyikondo, Diwani wa Kata ya Msoga, amesema mafunzo hayo yamewajengea uwezo mkubwa madiwani katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo usimamizi wa miradi ya maendeleo, fedha za umma na masuala ya utawala bora.







