📌Sweden, Norway wapongezwa kuwezesha utekelezaji wa mradi huo

📌Kituo kimejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 9.2

📌Kituo kinauwezo wa kutoa jumla ya megawati 18

📌Kamati ya Bunge ya Nishati waipongeza REA kwa utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini kikiwemo kituo kipya cha Mtera

📌Watanzania watakiwa kulinda miundombinu ya umeme

📍Mtera – Iringa

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imezindua Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Mtera (2x10MVA, 220/33kV) ambacho kitaongeza ubora wa umeme, kupunguza changamoto ya umeme mdogo na kuboresha huduma za kijamii, afya, elimu, maji na mawasiliano katika mikoa ya Iringa na Dodoma.

Akizungumza katika hafla hiyo leo Januari 16, 2026 mkoani Iringa, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema upanuzi wa kituo cha Mtera ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha nishati ya umeme inapatikana kwa uhakika na kwa gharama nafuu kwa wananchi katika maeneo ya vijijini.

Halikadhalika ameongeza kuwa, mradi huo utawanufaisha wananchi wa wilaya za Mpwapwa na Kongwa mkoani Dodoma, pamoja na wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, kwa kuboresha shughuli za kiuchumi na kijamii.

“Umeme upo wa kutosha, niwaombe wananchi wajitokeze kuunganishiwa umeme ili waweze kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotokana na upatikanaji wa nishati ya uhakika,” amesema Mhe. Ndejembi

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema REA imeleta mapinduzi makubwa katika kufikisha umeme vijijini, akibainisha kuwa mwaka 2014 ni asilimia 7 pekee ya wananchi wa vijijini waliokuwa na umeme, huku mwaka 2026 kiwango hicho kimefikia asilimia 78.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Simon Lusengekile, amepongeza mikakati ya Serikali kupitia REA katika kuwahudumia wananchi kupitia miradi ya nishati, huku akiwataka wananchi kulinda miundombinu ya umeme ili iweze kudumu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha, Mwakilishi wa Wabia wa Maendeleo ambao ni Norway na Sweden, Stephen Mwakifwamba, ambao wamechangia gharama za ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Mtera amesema kuwa wamefurahishwa na mafanikio ya utekeleza wa mradi ambao umeanza kuwanufaisha wananchi wa mikoa ya Iringa na Dodoma.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Meja Jenerali Mstaafu Mhe. Balozi Jacob Kingu, ameipongeza Menejimenti na watendaji wa REA kwa kukamilisha mradi huo kwa mafanikio, akisisitiza kuwa wakala una mchango mkubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya nishati nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mha. Hassan Saidy, amebainisha kuwa Kituo cha Mtera kimejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 9.2 na Serikali ya Tanzania kupitia REA kwa ushirikiano na Serikali za Sweden na Norway.

Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa ya Dodoma na Iringa, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amesema mradi huo utawanufaisha kwa kiasi kikubwa wananchi wa mikoa hiyo, huku akiipongeza REA kwa kazi kubwa ya kufikisha umeme vijijini.

Amesema licha ya kuwepo kwa umeme wa kutosha, matumizi ya sayansi na teknolojia ni muhimu katika kuhakikisha umeme haukatiki mara kwa mara, akiongeza kuwa miradi kama hiyo inaonesha mchango wa sayansi katika kupunguza changamoto za umeme.

Aidha, amewahimiza wananchi wa wilaya za Kongwa na Mpwapwa kutumia fursa ya umeme wa uhakika kuongeza uzalishaji wa viwandani na kuboresha uchumi wa Mkoa wa Dodoma kwa ujumla.