Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,
Dar es Salaam
Serikali imesema imejipanga kutoa elimu maalumu kwa Watanzania kuhusu fursa za uwekezaji ili kuongeza idadi ya miradi inayomilikiwa na wazawa na kupunguza utegemezi kwa wawekezaji wa nje.

Kauli hiyo imetolewa Leo January 16,2026 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, wakati akizindua kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani itakayotekelezwa kwa siku 60 nchi nzima.
Prof. Mkumbo amewahimiza wananchi wanaomiliki ardhi kuacha kuihifadhi bila matumizi na badala yake kuitumia katika shughuli za uzalishaji ili iwe chanzo cha kipato na kichocheo cha ukuaji wa uchumi wa taifa.
Amesisitiza kuwa kumiliki ardhi pekee bila mtaji, teknolojia au ushirikiano wa kibiashara hakumnufaishi mmiliki wala taifa, hivyo akashauri wananchi kuitumia TISEZA kuwatafutia wabia sahihi.

Prof. Mkumbo amewatahadharisha Watanzania kuacha tabia ya kukodisha majina yao kwa wawekezaji wa kigeni kwa maslahi madogo, akieleza kuwa hatua hiyo huwakosesha wazawa umiliki wa kweli na kudhoofisha uchumi wa ndani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Gilead Teri, amesema mamlaka hiyo imejiwekea lengo la kuvutia na kusajili miradi isiyopungua 1,500 katika kipindi kijacho.
Naye Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Kampuni ya Sukari ya Kilombero, Victor Byemelwa, ameipongeza serikali kupitia TISEZA kwa kuendelea kushughulikia changamoto za wawekezaji na kuboresha mazingira ya biashara.
Ziara ya kampeni hiyo inatarajiwa kuanza Januari 17, 2026, ikihusisha mikoa ya Tanzania Bara na Visiwani, huku elimu itakayotolewa ikilenga sekta za kipaumbele zilizoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.







