Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewahimiza Waumini wa Dini ya Kiislamu kutenda mambo mema ili kutajwa kwa wema ndani ya jamii pale wanapotangulia mbele ya haki.

Amesema hayo leo aliposhiriki Ibada ya Sala ya Ijumaa iliyosaliwa katika Msikiti wa Bamita Chumbuni, akisisitiza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kama sehemu ya juhudi za kutimiza matarajio ya wananchi.

Aidha, Sheikh Khalid Ali Mfaume, Katibu Mtendaji wa Afisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, ametoa wito kwa Waumini kuendelea kutafuta elimu ili kujijengea heshima ndani ya jamii.

Msikiti wa BAMITA uliwekewa jiwe la msingi mwaka 1981 na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Ali Hassan Mwinyi.

Alhaj Dkt. Mwinyi anaendelea na utaratibu wake wa kujumuika na Waumini wa Dini ya Kiislamu kwa kusali Sala ya Ijumaa katika misikiti mbalimbali mijini na vijijini.