Na Mwandishi wa OMH, Kibaha, Pwani
Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH), kwa kushirikiana na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), imeendesha mafunzo ya siku nne kwa watumishi wapya 20 walioajiriwa katika ofisi hiyo, kwa lengo la kuwajengea uwezo maalumu wa kiutendaji katika utumishi wa umma.
Mafunzo hayo ya siku nne yalifanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani, kuanzia Januari 13 hadi 16, 2026.

Mafunzo hayo yaliendeshwa na Mkurugenzi wa Utawala na usimamizi wa Rasilimali watu kutoka ofisi ya Msajili wa Hazina Bw. Chacha Marigiri, wakufunzi kutoka TPSC, wataalamu kutoka Hospitali ya Mnazi mmoja Pamoja na wataalaamu wa fedha na uwekezaji kutoka Mfuko wa Uwekezaji wa UTT AMIS.
Bw. Marigiri alitoa mafunzo kuhusu matumizi sahihi ya muda, akisisitiza umuhimu wa kuweka uwiano kati ya kazi na maisha binafsi ili kuepusha changamoto zinazoweza kumfanya mtumishi wa umma kushindwa kutekeleza majukumu yake.
“Watumishi wengi hushindwa kufanya kazi kwa ufanisi kwa sababu ya kukosa matumizi sahihi ya muda na kutoweka vipaumbele katika shughuli zao,” alisisitiza.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa TPSC, Bw. Hosea George ambaye ni mhadhiri kutoka chuo hicho alisema mafunzo hayo ni muhimu na mahususi kwa watumishi wapya ili kuwajengea uwezo wa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

“Mafunzo haya yanalenga kuchochea maendeleo ya serikali, pamoja na taasisi na mashirika ya umma yanayosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina,” alisema Bw. George.
Miongoni mwa mada zilizofundishwa ni pamoja na maadili na utendaji katika utumishi wa umma, Muundo wa serikali ya jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na uendeshaji wa shughuli zake kwa Tanzania bara na Zanzibar, mapitio ya sheria mbalimbali za utumishi wa umma, elimu ya afya ya ukimwi na magonjwa yasiyoambukizwa, afya ya akili, kupima utenda kazi wa watumishi pamoja na elimu ya fedha na kuweka akiba.
Akizungumza wakati wa kutoa mada ya afya, Dkt. Frank Mlaguzi kutoka Hospitali ya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam aliwataka watumishi wa umma kuzingatia utunzaji wa afya zao dhidi ya magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu, homa ya ini pamoja na changamoto za afya ya akili, akieleza kuwa magonjwa hayo huathiri kwa kiasi kikubwa utendaji kazi.
Bw. Chacha Marigiri aliwatunuku vyeti wahitimu wa mafunzo hayo na kukipongeza Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kwa kutoa mafunzo yenye tija, akibainisha kuwa mafunzo hayo yatasaidia kujenga watumishi wenye maadili, bidii na weledi.

Naye Goodluck Mtebene, mtumishi mpya wa umma katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, Kurugenzi ya Fedha na Uhasibu, aliishukuru Ofisi ya Msajili wa Hazina pamoja na TPSC kwa kuandaa mafunzo hayo.
“Mafunzo haya yamekuwa mwongozo muhimu katika kuufahamu vyema utumishi wa umma. Tunaahidi kuyazingatia maadili yote tuliyofundishwa katika utekelezaji wa majukumu yetu,” alihitimisha.





