Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Ruvuma

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mnyaa Mbarawa, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza zaidi ya shilingi trilioni 10.08 katika miradi 22 ya ujenzi, upanuzi na maboresho ya bandari kote nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha miundombinu ya usafiri wa majini na kukuza uchumi wa taifa.

Prof. Mbarawa ameyasema hayo tarehe 17 Januari, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Bandari mpya ya Mbamba Bay, iliyopo Wilaya ya Nyasa, Mkoa wa Ruvuma.

Akizungumza na viongozi wa Serikali, wataalamu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na wananchi wa eneo hilo, Prof. Mbarawa amesema uwekezaji huo mkubwa unaonyesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.

Ameeleza kuwa ujenzi wa Bandari mpya ya Mbamba Bay kwa shilingi Bilioni 81 ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotekelezwa chini ya Wizara ya Uchukuzi, hususani katika Maziwa Makuu, kwa lengo la kuimarisha biashara ya kikanda na usafiri wa majini katika Ziwa Nyasa.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA Mha. Dkt. Baraka Mdima, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, amesema mradi wa Bandari ya Mbamba Bay umefikia Asilimia 47 ya utekelezaji wake, na unaendelea kutekelezwa kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu, usalama na utunzaji wa mazingira.

Dkt. Mdima aliongeza kuwa kukamilika kwa bandari hiyo kutachochea biashara kati ya Tanzania na nchi jirani za Malawi na Msumbiji, sambamba na kuongeza ajira, uwekezaji na fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Wilaya ya Nyasa na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.

Naye Mhandisi Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay kutoka TPA, Bw. John Paul, alitoa maelezo ya kitaalamu kuhusu maendeleo ya mradi, akibainisha kuwa kazi zinaendelea vizuri na kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa.

Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas, aliipongeza Serikali kwa kuendelea kupeleka miradi mikubwa ya maendeleo mkoani humo, akisema bandari hiyo itakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa Nyasa na maeneo ya jirani.

Mradi wa ujenzi wa Bandari mpya ya Mbamba Bay unatarajiwa kuimarisha usafiri wa majini katika Ziwa Nyasa, kuchochea biashara kati ya Tanzania na Nchi jirani zikiwemo za Malawi na Msumbiji na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika biashara ya kikanda.