Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

WADAU wa Maendeleo wameombwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kubuni na kutekeleza miradi ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira nchini unaochangia upotevu wa misitu.

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Peter Msoffe wakati akizindua Mradi wa Kuongoa Ardhi na Kurejesha Uoto wa Asili Nchini Tanzania kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi, jijini Dodoma Januari 16, 2026.

Mradi huo unaofadhiliwa Serikali ya Ujerumani na kutekelezwa na Shirika la WWF Tanzania kwa kushirikiana na Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Mashirika ya International Union for Conservation of Nature (IUCN), World Resource Institute (WRI) na wadau mbalimbali na kutekelezwa katika Wilaya za Kilindi Korogwe (Tanga), Chamwino na Mpwapwa (Dodoma) zilizoathirika na uharibifu wa mazingira.

Prof. Msoffe amesema kuwa Serikali hii imezindua Dira ya Taifa ya Maendeleo -DIRA 2050 ambayo imetambua umuhimu Mazingira na kuweka Nguzo ya ‘Uhifadhi wa Mazingira na Ustahimilivu wa Mabadiliko ya tabianchi’ ambayo inakumbusha kutunza mazingira na kubuni miradi itakayotoa majawabu ya changamoto zinazoikabili nchi.

Alisema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Makubaliano ya Changamoto ya Bonn yaliyofikiwa mwaka 2011 jijini Bonn nchini Ujerumani kuwa dunia inapaswa kuongoa hekari milioni 350 za misitu ifikapo mwaka 2030 na Tanzania imeahidi kuongoa hekari milioni 5.2 kupitia mpango wa AFR100.

“Sote tunafahamu kuwa uoto wa asili ni rasilimali muhimu kwa ustawi wa mazingira na maisha ya binadamu, huchangia katika uhifadhi wa vyanzo vya maji, kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, kulinda bioanuwai na pia kutoa fursa za kiuchumi kwa jamii. Hata hivyo, changamoto hizo kutokana na shughuli zisizo endelevu za kibinadamu zimeendelea kuathiri mazingira yetu na binadamu wenyewe, hivyo mradi huu umekuja kwa wakati muafaka ili kuisaidia Serikali kuhimili na kukabiliana na changamoto hizo,” alisema Prof. Msoffe.

Aliongeza kuwa mradi huo unalenga kurejesha mifumo ikolojia kwa kuhusisha jamii kikamilifu na hivyo kutarajiwa kuwa na mazingira wezeshi ya kisera n a mikakati mahsusi ya kuhakikisha kuwa jamii nzima inashiriki katika kurejesha uoto wa asili nchini kwani miradi inayohusisha jamii moja kwa moja imekuwa na mafanikio makubwa hivyo kuleta mabadiliko chanya.

Mradi wa Kuongoa Ardhi na Kurejesha Uoto wa Asili unatarajiwa kutekelezwa katika Wilaya za Kilindi Korogwe (Tanga), Chamwino na Mpwapwa (Dodoma) ambapo haya ni maeneo yaliyoathirika kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa mazingira.

Takwimu zinaonesha kuwa kati ya mwaka 2001 na 2024 Wilaya ya Kilindi ilipoteza takriban hekta 32,000 za misitu (sawa na asilimia 21 ya misitu yote ya mkoa wa Tanga iliyopotea katika kipindi hicho.
Hivyo, Prof. Msoffe aliwashukuru wadau wa maendeleo WWF, IUCN na WRI kwa kukubali kutekeleza mradi huo nchini Tanzania.

Kwa upande wake Meneja wa Uhifadhi wa WWF Tanzania Dkt. Lawrence Mbwambo alisema mradi huo umejikita katika eneo la kurejesha uoto wa asili kwenye kilimo, ufugaji, mito na mazingira kwa ujumla.

Aliishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kufanya kazi bega kwa bega na shirika hilo katika hatua mbalimbali za kuhakikisha hifadhi ya mazingira inakuwa endelevu.

Dkt. Mbwamo alisema kuwa WWF imekuwa ikifanya kazi na Ofisi ya Makamu wa Rais katika shughuli mbalimbali zikiwemo kuandaa Mkakati wa Kupambana na viumbe vamizi ambao unaendelea kutekelezwa.

Alisema shirika hilo lipo tayari kufanya kazi na Serikali katika kuhakikisha mradi huo unakuwa endelevu na kuleta tija kwa jamii hususan katika maeneo ambayo yamenufaika nao.

Naye Mwakilishi wa Kamishna wa Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzannia (TFS) Bw. Hamza Kateti alisema jukumu la kuongoa ardhi linahitaji ushirikishaji wa wadau zikiwemo taasisi.

Alisema juhudi hizi zitasaidia kutimiza azma ya Serikali ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira kwa ujumla ambao unaleta madhara kwa sekta mbalimbali za uchumi.