Na Allan Kitwe, JmahuriMedia, Tabora

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Magharibi imefanya oparesheni maalumu na kufanikiwa kukamata dawa zenye thamani ya sh mil 822.8 zilizokuwa zinauzwa kinyume na utaratibu.  

Hayo yamebainishwa jana na Meneja wa TMDA Kanda ya Magharibi, Christopher Migoha alipokuwa akiongea na waandishi wa habari, ambapo alieleza kuwa jumla ya kilo 2,300 zenye thamani ya shilingi mil 822.8 zimekamatwa na kuteketezwa.

Alifafanua kuwa dawa na vifaa tiba hivyo vimekamatwa katika oparesheni maalumu iliyofanyika katika hospitali, vituo vya afya, zahanati na maduka ya dawa baridi za binadamu na mifugo katika Wilaya zote.

Migoha alieleza kuwa dawa hizo haziruhusiwi kuuzwa katika maduka ya watu binafsi na ni kinyume cha sheria na kanuni ya 63 ya mwaka 2005 ya dawa zilizozuiliwa kuuzwa hadharani hususani katika maduka ya watu binafsi.

Aliongeza kuwa katika operesheni hiyo walikagua jumla ya maduka 408 ya dawa, Hospital 16, vituo vya afya 17, zahanati 17, famasi 66, maduka ya dawa muhimu za mifugo 37 na maduka ya dawa muhimu za binadamu 230.

Maeneo mengine ni maghala ya kuhifadhi dawa za binadamu 2, kliniki za kibingwa 1, kliniki ya mifugo 1, magari ya kubebea dawa za binadamu na mifugo 20 na  maeneo ya uzalishaji maji Tiba 2

Aidha aliongeza kuwa walikamata baadhi ya dawa ambazo ni salama lakini hazistahili kuuzwa kwenye maduka hayo na kuzigawa kwenye baadhi ya Hospitali za umma ikiwemo kuondoa sokoni baadhi ya dawa.

Migoha alidokeza kuwa mbali na tukio hilo watumishi wa taasisi hiyo pia wamejumuika kwenda kutoa msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya sh mil 28.2 kwa hospitali ya Jeshi la Wananchi ya Milambo iliyoko Mkoani hapa.   

Naye Afisa Lishe wa Mkoa huo, Paulo Makali, akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa huo, aliwataka wauzaji na wasambazaji wa dawa kununua dawa kwenye maeneo rasmi ili kuepuka kubabikwa .

Baadhi ya wadau wa TMDA, walishauri kufanyika semina za mara kwa mara kwa wauzaji wa dawa hizo ili kukumbushana juu ya namna bora ya uuzaji wa dawa na vifaa tiba ili kuokoa afya za watumiaji.