Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Serikali kupitia wizara ya afya imeweka mkakati wa kujenga na kuimarisha viwanda vya dawa ili kulifanya taifa kujitegemea katika
uzalishaji dawa,vifaa tiba na chanjo.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, ameyasema hayo katika mkutano wa
wawekezaji wa viwanda vya dawa na vifaa tiba uliofanyika Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.
Amesema Serikali imeanza kutekeleza ajenda ya kuwa na viwanda vya dawa na vifaa tiba, ili kuhakikisha bidhaa hizo zinazalishwa kwa wingi na viwanda vya ndani, jambo ambalo litachochea maendeleo ya nchi.
Mchengerwa amesema Serikali ina mpango mkakati wa kujenga na kuimarisha viwanda vya dawa ili kulifanya taifa lijitegemee katika
uzalishaji wa dawa, vifaa tiba na chanjo ili kulifanya liwe salama.
Amesema Wizara ya Afya imejipanga kutekeleza maelekezo ya Rais sambamba na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, inayolenga nchi kujikita katika uzalishaji wa dawa na vifaa tiba ndani ya nchi kwa ajili ya kulinda usalama wa afya na uhuru wa taifa.
Serikali pia imetenga takribani Dola za Marekani milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya kisasa , itakayotumika kufanya tafiti na kupima viwango na ubora wa dawa zinazozalishwa nchini.
Amesema kwa sasa Tanzania huzalisha chini ya asilimia 10 ya mahitaji ya dawa, ingine ikiagizwa kutoka nje, hali inayoweza kuwa hatari hasa wakati wa majanga ya kimataifa.
“Ni muhimu taifa lijitosheleze katika uzalishaji wa dawa, kwa sababu kuagiza kutoka nje kunaweza kuhatarisha usalama wa afya ya wananchi,” amesema Mchengerwa.

Amesema Serikali inalenga kuongeza uzalishaji wa dawa kutoka chini ya asilimia 10 ya sasa hadi kufikia kati ya asilimia 65 hadi 80 ifikapo mwaka 2030, linawezekana kutokana na mipango na uwekezaji unaoendelea.
Aidha, Serikali imesema imeanza kuweka mifumo ya kuunganisha tiba asilia na tiba za kisasa, ikizingatiwa kuwa zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania hutumia tiba asilia.
Hatua hiyo itaenda sambamba na utekelezaji wa bima ya afya kwa wote,
Ametaja hatua ambazo tayari serikali imezitekeleza, akieleza mojawapo
ni ujenzi wa kituo cha uzalishaji dawa cha Mloganzila na Kibaha mkoani Pwani.
Waziri Mchengerwa amesema kuwa vituo hivyo vinajumuisha na kuwaleta pamoja wazalishaji wa bidhaa za dawa na vifaa tiba, wasimamizi wa sekta hiyo, watafiti pamoja na miundombinu ya usafirishaji.
Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji wa Madawa nchini, Bashiri Haroun , amesema uamuzi wa Serikali kuimarisha sera na mazingira ya uwekezaji kwenye viwanda vya dawa ni fursa kubwa kwa wazalishaji wa ndani, kwani utaongeza ushirikiano na wawekezaji wa kimataifa pamoja na matumizi ya teknolojia ya kisasa.
Haroun amesema wazalishaji wa dawa wamewekeza kwenye viwanda
mbalimbali, lakini changamoto kubwa iliyokuwapo awali ilikuwa ni sera.
Alieleza kuwa maboresho ya sera yanayoendelea yanaonesha dhamira ya
dhati ya Serikali kulinda na kukuza viwanda vya ndani.
“Hii ni fursa kubwa kwetu wazalishaji wa dawa, kwa sababu sasa tunakwenda kupata wawekezaji wa nje watakaotuunga mkono, kuongeza ushirikiano na kuleta teknolojia ya juu zaidi,” amesema Haroun.
Aliongeza kuwa kuundwa kwa timu maalum na Waziri pamoja na mwaliko kwa wawekezaji wa nje kunaonesha nia ya Serikali kushughulikia changamoto zote zilizokuwapo na kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji.
Haroun amesema eneo la Mloganzila kuwa ni kitovu muhimu cha uwekezaji kutokana na miundombinu iliyowekwa na Serikali ikiwemo umeme, maji na gesi, akisema hatua hiyo itachochea ukuaji wa viwanda vya dawa, vifaa
tiba na chanjo.
