Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Heri ya mwaka mpya 2026. Narejea katika safu hii baada ya gazeti letu kutokuchapishwa kwa wiki tatu mfululizo kuanzia Desemba 30, 2025.
Kwanza, ninawashukuru sana wasomaji wetu kwa simu, maombi na matashi mema juu ya uendelevu wa Gazeti letu la uchunguzi la JAMHURI.
Desemba 31, 2025 tulitoa taarifa ya kusitisha uchapishaji wa gazeti hili kutokana na madeni makubwa yanayotukabili.
Sitanii, tunawashukuru watangazaji wetu walioguswa na kuamua kutulipa kwa mkupuo, hali iliyopunguza madeni yetu kwa kiasi kikubwa na sasa tunarejea sokoni.
Nimeyaona mapenzi makubwa ya Watanzania juu ya Gazeti la JAMHURI na niseme bayana kuwa tumerudi kuwatumikia na kuijenga nchi yetu kwa masilahi mapana ya umoja, mshikamano, amani, upendo na maisha bora kwa Watanzania.
Kimsingi niseme sijapata muda mzuri wa kuchambua hali tuliyomo sasa kama nchi. Nimetumia muda wa kutokuwa sokoni kama sehemu ya mafungo na kuwaza cha kufanya.
Nilipata kuandika mara nyingi katika makala zangu zilizotangulia kuwa Tanzania si tofauti na majirani zetu. Nilisema kuwa amani tuliyonayo tuitunze, hatuioni kama ina thamani kwa kuwa tunayo, ikituponyoka tutajuta.
Niliandika pia kuwa sisi Watanzania tulipata uhuru kwa njia ya mazungumzo. Wengi wetu tuliamini kuwa yaliyotokea Oktoba 29, 2025 yasingeweza kutokea Tanzania. Wengi waliamini Tanzania na Watanzania tuna vinasaba tofauti kabisa na majirani zetu ambao kwao kupigana na kuuana si jambo geni. Tulilodhani haliwezekani, sasa tumekwishashuhudia kuwa linawezekana katika ardhi ya Tanzania.
Sitanii, nilionya kuwa matendo yetu ni mauti yetu iwapo tusingefunga breki katika kuhamasishana kutunishiana msuli, hili halikusikika.
Nilieleza kuwa hatuhitaji kuanzisha ugomvi tukafarakana kisha tutafute mtu wa kutusuluhisha turudi katika amani. Bahati mbaya, maneno haya hayakupenya kwenye masikio ya baadhi ya Watanzania, waliodhani wakati umefika wa kupitia njia mbadala kupata uongozi.

Kwa upande wa serikali na chama tawala, nako niliandika nikasema uchaguzi unapofanyika basi uwe huru na wa haki. Kwamba isifike mahala wakati tunakwenda kwenye uchaguzi mshindi akawa amekwishafahamika.
Nilisema yaliyotokea mwaka 2019, 2020 na 2024 ya wapinzani kuchukuliwa kuwa hawajui kusoma na kuandika, hayana afya kwa ustawi wa demokrasia na taifa letu.
Nilisema tulikokuwa tumefika hali ya watu kukamatwa na wakapotea kama kuku aliyenyakuliwa na kicheche bila maelezo ya uhakika, kulikuwa kuna momonyoa misingi ya amani yetu tuliyoachiwa na waasisi wa taifa letu; Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume. Demokrasia ni msingi wa maendeleo, kwamba wagombea wa vyama vya siasa katika ngazi zote wawe na nafasi sawa ya kushinda na kushindwa.
Sitanii, nilikutana na wapinzani akiwamo Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wa sasa, Tundu Lissu, nikawaambia siasa za hoja zinalifaa zaidi taifa letu kuliko harakati za ‘kukinukisha’. Niliwaambia kuwa kuingiza watu barabarani kungepoteza maisha na mali, hali inayotishia uhai na umoja wa taifa letu. Niliwaasa juu ya kauli zenye kuashiria shari, ila sikusikilizwa.
Viongozi wa dini nilinena nao kwa upole na unyenyekevu mkubwa, nikazisihi dini zetu zote, Wakristo, Waislamu na madhehebu mengine kujiepusha na lugha kali zenye kuashiria mbinyo kwa dini au upande mwingine. Ilifika mahala nikaona majibizano ya viongozi wa dini hadi nikaogopa. Namshukuru Mungu kwa wiki tatu hizi nilizokuwa kwenye mafungo, si Wakristo, wala Waislamu walioendelea na lugha kali zilizotishia amani.
Sitanii, yote niliyotabiri yametokea. Nilisema tukianza kukejeli dini za wengine, tutalitumbukiza taifa kwenye sintofahamu ya hali ya juu.
Nafikiri sote tu mashahidi juu ya viongozi kadhaa wa dini na ‘waigizaji’ waliojifanya ni Wakatoliki kupeleka barua kwa mwakilishi wa Papa nchini, kisha wakajikuta wanakosea si mavazi tu, bali hata sala na nyimbo walizokuwa wakitumbuiza. Tuliwasikia waliohamasisha tukatane vichwa!
Binafsi naomba nisisitize hapa. Mkatoliki asimkejeli Mwislamu. Mkatoliki asimkejeli mwamini wa KKKT, wala Mwislamu asimkejeli Mkatoliki, Anglikana au Walokole wasiwashambulie dini na madhehebu mengine. Sisi tuendelee kuishi kama Watanzania. Tupendane, tujenge taifa imara lenye umoja, upendo na mshikamano.
Najua litakuja swali kwamba hapa tulipofika tunatokaje? Rais Samia Suluhu Hassan ameunda Tume ya Uchunguzi chini ya Jaji Mkuu (mstaafu), Mohamed Chande Othman. Rais Samia amesema baada ya matokeo ya tume hii iliyopewa miezi mitatu, mchakato wa maridhiano kama nchi utaanza. Tumesikia Rais pia katika hotuba yake ya kufungua mwaka wa mabalozi nchini pale Ikulu Dodoma wiki iliyopita. Hakuuma maneno. Ameeleza nia thabiti ya kuwaunganisha tena Watanzania.
Sitanii, napigiwa simu na baadhi ya watu, tena wengine ni wasomi wakubwa tu – madaktari na maprofesa wakitaka tuweke shinikizo awepo mtu kutoka nje ndiye asimamie maridhiano. Kwa uzoefu wangu wa karibu miaka 32 kazini, maridhiano yatakayotokana na Watanzania wenyewe (home grown solutions) yanayo nafasi kubwa ya kuwa na ufanisi kuliko maelekezo (prescriptions) kutoka nje ya nchi. Zanzibar walipata kujaribiwa, akaletwa Chief Emeka Anyaoku kutoka Nigeria aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola mwaka 1998/1999 kuwasuluhisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF). Ilishindikana.
Mwaka 2010, walikaa Watanzania wenzetu; Rais Dk. Amani Abeid Karume na Maalim Seif Shariff Hamad wa CUF wakati huo, wakalimaliza. Hawa waliingia mwafaka, wakaunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). Najua zipo cheche za hapa na pale Zanzibar, ila hauwezi kuzilinganisha na moto uliokuwapo enzi hizo. Kadiri wanavyoendelea na mazunguzo naiona Zanzibar ikiishaukubali utamaduni huu, SUK imeleta utangamano.
Sitanii, nyakati za uchaguzi tulizoea kusikia Wazanzibari wanatafutana. Wengi walikuwa wanakimbili Dar es Salaam. Zamu hii imekuwa kinyume. Wengi wametoka Dar es Salaam kukimbilia Zanzibar. Kumbe inaonyesha maridhiano ni jambo la msingi. Katika maridhiano naona kesi nyingi ikiwamo inayomkabili Lissu zikifutwa. Haitakuwa ya kwanza kwani hata walioandamana Oktoba 29, 2025 wengi walifunguliwa kesi za uhaini, lakini Rais Samia amezifuta.
Hapo juu nimezungumzia siasa za sera. Natamani kuona nchi yetu ikirejea katika siasa za nguvu ya hoja, badala ya hoja ya nguvu. Maneno nchi hii ni yetu sote, tumeyasikia mara nyingi. Nani alijua Patrobas Katambi aliyekuwa anapigwa virungu na polisi leo angekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani? Yaani bosi wa polisi walewale waliokuwa wanamtwanga virungu?
Natamani tuwe na Tanzania aliyoilenga Mwalimu Nyerere. Tukatae udini, tukatae ukabila, tukatae umajimbo, jinsia, Uzanzibari, Uzanzibara na Utanganyika.
Tuepuke kujenga chuki dhidi ya watu wanaofanya kazi kwa uadilifu wakapata fedha. Kuwa maskini si sifa, hivyo mtu aliyepata utajiri kwa njia halali tusimjengee chuki mbele ya jamii. Tunatafuta maisha bora kwa kila Mtanzania, lakini pembeni tunahamasisha watu wachome mali za matajiri.
Sitanii, siasa za kudhani tukiwatukana watoto wa wakubwa au kuwachonganisha na jamii zitamaliza matatizo yetu, hazitatufikisha popote. Siasa za kumfungulia mashitaka kila anayekukosoa au kuikosoa serikali hazitatufikisha popote.
Viongozi wa kisiasa nao wawe sehemu ya maridhiano. Lugha za kejeli, matusi na ubabe, hazitatusaidia kubadili maisha ya Watanzania. Nimeyasema haya nikirejea uzoefu. Marais wetu wakiwa madarakani tuna hulka ya kuwachukia na sijui ilianzia wapi!
Mwalimu Nyerere wakati akiwa Rais ukitaka kujua kuwa baadhi ya watu walimchukia, alinusurika kupinduliwa mara mbili au zaidi. Mwaka 1963 na mwaka 1982. Hauwezi kusema hadi yanafanyika majaribio haya hakukuwapo chuki iliyojengwa. Walimwita ‘Mchonga’.
Baada ya hapo kwa tuliokuwapo, Mzee Ali Hassan Mwinyi kwa kaulimbiu yake ya ‘Ruksa’, alikejeliwa kila kona. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia jarida lisilo rasmi la ‘Punch’ lilimchora mara kadhaa kama nyoka, mara kama kiboko…
Mama Siti akageuzwa mbuzi wa kafara, maandamano yalikuwa mengi hadi akakifunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam baadhi ya wanafunzi wakapoteza sifa za kuendelea na masomo. Kama haujui muulize James Mbatia, analifahamu hili.
Mzee Benjamin Mkapa alipoingia madarakani, nchi nzima tukawa tunaimba wimbo wa ‘UKAPA’. Marehemu John Komba alikuwa ‘amefyatua kibao’ chake cha ‘Mtaji wa Maskini ni Nguvu Zake Mwenyewe’, majambazi wakautumia wimbo huu kama fursa. Magari yalitekwa hadi ikapitishwa amri ya magari kutosafiri usiku. Mzee Benjamin Mkapa alitukanwa kila kona. Leo magari yanasafiri saa 24!
Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, alitoa uhuru wa kila awaye kufanya atakacho. Hili nalo likageuzwa kuwa kero. Watanzania tukamkejeli kuwa ni ‘Mzee wa Kubembea’. Wizi kwenye benki ilikuwa haipiti siku mbili bila kusikia taarifa za majambazi kuingia benki wakaiba fedha. Mtoto wake Ridhiwani akawekwa kwenye rada ya Watanzania. Kila jengo, kituo cha mafuta, basi au mradi uwao, tuliambiwa ni vya Ridhiwani.
Sitanii, Rais John Pombe Magufuli alipoingia madarakani akabana matumizi. Akasema Sh 500 mtaacha kuiita ‘jero’. Ukaja msamiati wa ‘Vyuma Vimekaza’. Wakaja wasiojulikana. Akaunti za watu zikawa zinaporwa fedha na mamlaka za nchi bila maelezo. Wawekezaji wakaikimbia nchi yetu. Makusanyo ya kodi yakashuka, hadi miradi ya ujenzi iliyoanzishwa kama barabara ya Nansio – Ukerewe na nyingine zikasimama. Kariakoo madalali wakaanza kutafuta wateja wa kupangisha fremu. Kariakoo, si Mbagala!
Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere (Mungu ambariki Magufuli kwa kuuanzisha), makandarasi kutoka Misri wakafika mahala wakawa wanadai ukaelekea kusimama. Reli ya SGR Dar – Morogoro ikasuasua kuanza kwa sababu vilinunuliwa vichwa chakavu Ulaya, vikashindikana kukarabatiwa. Kila mtu akawa analia ukata.
Sitanii, kinachoshangaza, leo ukisikiliza Watanzania wale wale waliokuwa wanawaona Rais Nyerere, Rais Mwinyi, Rais Mkapa, Rais Kikwete na Rais Magufuli ‘hawafai’, leo wanakutajia mazuri na kuwashuhudia kama wana wa nchi hii wanaostahili kujengewa minara.
Watu wanasimulia watangulizi wa Rais Samia na kuonyesha kama wale walikuwa malaika walioshuka kutoka mbinguni. Najiuliza, ilikuwaje wakati wapo madarakani hawakuonekana kuwa viongozi wa maana hadi baadhi wakajaribu kumpindua Nyerere? Nini kimetokea leo tunawanukuu katika kauli na maandiko yetu tukiwataja kama mashujaa? Wanaonijibu ni wachache.
Leo ni zamu ya Rais Samia Suluhu Hassan. Wapo watu wanamshushia kila tuhuma na kuikejeli familia yake, lakini atakapomaliza uongozi nchi ikiwa na umeme megawati zaidi ya 8,000, historia ya Bwawa la Mwalimu Nyerere aliloanzisha Rais Magufuli akaliacha katika asilimia 30 yeye akalijenga na kulikamilisha, GSR ikifika Mwanza – Burundi na DRC, wanafunzi wote wa vyuo vikuu na vya elimu ya kati kupewa mikopo…
Elimu ya msingi ikawa inafikia kidato cha nne, vijiji vyote nchini vipata umeme/maji, vituo vya afya kuwa katika kila kata, barabara za vijijini kupitia TARURA zikajengeka vizuri, Dar es Salaam ujenzi wa barabara za mwendokasi na mitaa unaoendelea ukakamilika chini ya DMDP na mengine mengi, utasikia matusi atakayoyakoga Rais ajaye kuwa mbona Rais Samia aliweza yeye anashindwaje?
Wakati nahitimisha makala hii, nasisitiza. Tuimarishe demokrasia na mfumo wa vyama vingi uonekane kuwa unafanya kazi. Viongozi wa kisiasa wasihamasishe vurugu kupitia kauli sizizo na staha. Tuepuke migogoro ya kidini. Kama sehemu ya maridhiano, kesi zote zenye sura za kisiasa zifutwe.
Tuwe watu wa kusikilizana na kuheshimu wenzetu bila kujali jinsia. Naamini tumejifunza kwa yaliyotokea na tunayo nafasi ya kuijenga upya nchi yetu. Mwaka 2026 tuutumie kujenga tulipoharibu. Mungu ibariki Tanzania.
0784 404827


