Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Nzega
MWANAMKE mmoja ambaye jina halijajulikana amejifungua mtoto na kumtelekeza kwenye nyumba ya kulala wageni (gesti) Wilayani Nzega mkoani Tabora na kutokomea kusikojulikana.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Mkuu wa Wilaya hiyo Naitapwak Tukai ameeleza kusikitishwa na tukio hilo na kuahidi kutoa donge nono la shilingi 500,000 kwa mtu yeyote atakayesaidia kupatikana mwanamke huyo.

Alieleza kuwa kitendo hicho hakikubaliki katika jamii na ni ukatili wa hali ya juu, kama huyo mama aliweza kukaa na mimba kwa miezi yote tisa na kujifungua salama iweje amtupe mtoto gesti?, alihoji.
‘Naomba mtu yeyote mwenye taarifa za mwanamke aliyekuwa mjamzito na sasa haonekani kuwa na mtoto atoe taarifa Kituo cha Polisi au aje kwa Mkuu wa Wilaya moja kwa moja anipe taarifa, hatutamtaja kokote’, alisema.
DC alibainisha kuwa mtoto anakadiriwa kuwa na umri wa siku 3 tu tangu azaliwe, hivyo kumtelekeza namna hii ni kumnyima haki yake ya msingi ya kunyonya maziwa ya mama, kupata malezi yake na kukwepa majukumu.
Akizungumizia tukio hilo, mhudumu wa gesti hiyo iliyoko Mtaa wa Ntinginya Mjini Nzega, Christina Kahema alieleza kuwa mama huyo alifika hapo majira ya saa 1.30 jioni na kuomba chumba akiwa amejifunika kitenge na kupakata mtoto.

Mhudumu aliongeza kuwa alipotoka kidogo kwenda kumwonesha chumba mteja mwingine aliporudi hakumkuta, alikuta kichanga kimelazwa sakafuni hapo mapokezi na mama hakuonekana tena, wakakichukua na kukipeleka Polisi.
Daktari wa zamu wa Hospitali ya Wilaya Dkt Davis alisema kuwa walimpokea mtoto huyo wa kike mwenye uzito wa kilo 2 walipomchunguza hawakuona changamoto yoyote hivyo wakampa dawa za antibiotiki kuzuia wadudu na kumwanzisha vyakula vyenye virutubisho kulingana na umri wake.



