Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

WATU wanne wamekamatwa na Jeshi la Polisi Mkoani Tabora kwa tuhuma za kuhujumu Mradi wa Maji wa Miji 28 unaoendelea kutekelezwa na serikali katika Wilaya za Sikonge, Urambo na Kaliua ili kumaliza kero ya wananchi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani hapa ACP Constatine Mbogambi amethibitisha kukamatwa watuhumiwa hao wakiwa na vifaa mbalimbali vilivyoibiwa kwenye mradi huo Wilayani Urambo.

Alitaja baadhi ya vifaa vya mradi huo vilivyokamatwa kuwa ni mashine kubwa 3 za kuchomelea mabomba, grenda mashine 2 za kukatia mabomba, nyaya 9 za kuunganishia grenda hizo na lita 40 za mafuta ya mitambo ya hydroliki.

Kamanda alifafanua kuwa vifaa hivyo viliibiwa usiku wa tarehe 11 Januari 2026 Wilayani Urambo katika eneo la mradi huo mkubwa wa maji kutoka ziwa Victoria ambao unatekelezwa na serikali kwa gharama ya zaidi ya sh bil 143.

‘Baada ya kuibiwa mashine na vifaa hivyo, vilisafirishwa na kwenda kufichwa katika Kitongoji cha Ubalani-Majengo, Mjini Urambo tayari kwa ajili ya kutafuta wateja ili kuwauzia’, alisema.  

Alidokeza kuwa watuhumiwa hao watapandishwa kizimbani muda wowote kuanzia sasa ili kujibu tuhuma zinazowakabili za kuhujumu miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali kwa gharama kubwa.

Wakati huo huo Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani hapa amethibitisha pia kukamatwa watu watano wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya wizi wa pikipiki za abiria katika Mikoa ya Tabora na Shinyanga.

Alieleza kuwa katika msako uliofanyika Januari 6 na 7 mwaka huu jumla ya pikipiki 9 za wizi zenye thamani ya zaidi ya shilingi 24 zilikamatwa katika Wilaya ya Nzega na Kahama, watuhumiwa wote tayari wamefikishwa mahakamani.

Kamanda Mbogambi amebainisha kuwa Jeshi la Polisi Mkoani hapa limejipanga vizuri, litaendelea kukabiliana na vitendo vya uhalifu wa aina yoyote ile na waharifu wote watashughulikiwa ipasavyo.