Watu wasiopunguwa 114 wamefariki na uharibifu mkubwa wa mali umeripotiwa huku baadhi ya vijiji vikifunikwa kabisa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa nchini Msumbiji.
Timu ya waokoaji nchini Msumbiji inaendelea kutafuta watu walionusurika baada ya mafuriko mabaya kuwahi kuikumba nchi hiyo. Takriban watu 114 wamekufa tangu ulipoanza msimu wa mvua mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka jana.
Mafuriko mabaya ambayo hayajawahi kuonekana kwa miongo nchini humo,yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha yameharibu vijiji kadhaa.
Umoja wa Mataifa umesema maji yanayoongezeka yamesababisha hali ya dharura , katika mkoa wa Kusini mwa Maputo timu ya msaada wa dharura imetembelea eneo kubwa lililofunikwa kabisa na maji wakiwatafuta wakaazi waliokwama pamoja na kutathmini uharibifu uliotokea Msumbiji.
Umoja wa Mataifa jana ulisema zaidi ya watu nusu milioni katika nchi hiyo ya wakaazi kiasi milioni 35 wameathirika.



