Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kilimanjaro
BODI ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi ( AGRB) imekabidhi zawadi za zaidi ya Sh.milioni 6.8 kwa washindi wa shindano la Insha kwa mwaka 2024/25 huku ikiwataka wanafunzi kusoma zaidi masomo ya sayansi
Akizungumza kwenye zoezi la kukabidhi zawadi kwa shule za msingi na sekondari zilizoshiriki shindano hilo kwa mkoa wa Kilimanjaro Ofisa Uhusiano wa AQRB Hamisi Sungura amesema shindano hilo linalenga kuhamasisha wanafunzi waweze kuzijua fani hizo na faida zake kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Akikabidhi zawadi ya ushindi wa sh.300,000 kwa shule ya Anwarite inayomilikiwa na Jimbo Katoliki Moshi ambayo imeshinda kwa
wanafunzi wake kujitokeza kwa wingi kwenye shindano hilo Sungura amesema bodi imehamadika kutoa zawadi hiyo kwa kutambua ushawishi mkubwa uliofanywa na walimu
Aidha ameuomba uongozi wa shule hiyo kuendelea kuhamasisha wanafunzi kupenda kusoma masomo ya sayansi ili waweze kuwa wataalamu wa fani hizo hapo baadaye ili kuliwezesha taifa kuwa na wataalamu wa kutosha
” AQRB Leo tunaukabidhi uongozi wa Shule ya wasichana Anwarite fedha hizo kwa kutambua mchango mkubwa uliofanywa na walimu katika kuhamasisha wanafunzi kushiriki shindano hilo,” amesema Sungura na kuongeza kufanya hivyo itakuwa ni chachu kwa shule zingine kuiga mfano huo na kujitokeza kushiriki kwa wingi
Pia Sungura amesema Bodi ya AQRB imemkabidhi zawadi ya Sh. 100,000 mwanafunzi Emiliana Lyamuya wa shule hiyo kwakuwa mmoja wa washindi wa mkoa katika shundano hilo kwa mwaka 2024/25 na kumtaka kutimiza ndoto zake za kuwa mtaalamu wa fani za Ubunifu na Ukadiriaji Majenzi.

Kwa upande wake Mbunifu Majengo kutoka AQRB Halima Mrisho amewapatia elimu wanafunzi juu ya umuhimu wa fani hizo katika muskakabali wa maendeleo ya nchi katika Sekta ya Ujenzi
Amesema katika taifa lolote ili kuwa na miundombinu bora katika Majenzi lazima wataalamu wa Ubunifu na Wakadiriaji Majenzi wahusishwe
“Tumeona ni kwa namna gani serikali imekuwa ikihakikisha miradi yote mikubwa ya kimkakati ikiwahusisha wataalamu wa fani hiyo,hivyo ni muhimu vijana mkaona umuhinu wa kutamani kuwa wataalamu wa fani hizi,” amesema Mrisho.

Ofisa Elimu Katà ya Kirua Vunjo Kusini Hassan Msheri amefurahishwa na ushindi wa shule hiyo na kuwasisitiza wanafunzi wengine pale zinapotokea fursa za aina hiyo kijitokeza kwa wingi kwa lengo la kushinda na kujifunza zaidi
Hata hivyo Mkuu wa Shule hiyo Sista Secilia Shao ameahidi kuendelea kushirikiana na uongozi wa bodi katika kuhamasisha wanafunzi kupenda kusoma masomo ya sayansi hususan fani za Ubunifu Majengo na Ukadiriaji Majenzi ili kuliwezes ha taifa kuwa na wataalamu wa kutosha katika fani hizo.




