Na WAF, Dodoma 

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Idara ya Afya ya Uzazi wa Mama na Mtoto, kwa kushirikiana na Shirika la Thamini Afya wamekutana pamoja na kuweka mikakati utekelezaji wa Mradi wa Ushirikiano wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi. 

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Dkt. Ahmad Makuwani wakati wa kikao hicho kilichofanyika leo Januari 21, 2026 katika Ofisi za Wizara ya Afya Mtumba jijini Dodoma.

“Serikali imeweka nia ya dhati ya kuhakikisha inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi kwa kushirikisha wadau mbalimbali ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huo,” amesema Dkt. Makuwani 

Ameongeza kuwa ni muhimu kwa Wizara ya Afya kupitia Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto ikuweka mikakati bora ya namna ya kutekeleza mradi huo ikiwa ni pamoja na kuangalia maeneo yanayopaswa kupewa kipaumbele katika mradi huo ikiwemo ujenzi wa majengo ya uangalizi maalum wa mtoto wenye changamoto mbalimbali (NICU) na kuongeza idadi vifaa tiba vya kisasa vitakavyosaidia utoaji wa huduma hususan wakati wa kujifungua. 

Aidha, amesema kuwa ni muhimu kutoa mafunzo kwa wadau wengine ikiwemo wasisimamizi watakaoshiriki katika mradi huo ili kuhakikisha unatakelezwa kwa ufanisi wa hali ya juu. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi kutoka Shirika la Thamini Uhai na Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya kina mama na uzazi Dkt. Sunday Dominico amesema kuwa, utekelezaji wa mradi huo ni wa kipindi cha miaka 5 ukihusisha mikoa 3 ya Kigoma, Katavi na Geita. 

“Shirika la Thamini Uhai limepata nafasi ya kutekeleza mradi wa ushirikiano baina ya serikali na wadau wa maendeleo unaolenga kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto hususani katika kipindi cha kliniki na wakati wa kujifungua”, amesema Dkt. Sunday. 

Ameongeza kuwa, mradi huo unalenga pia kutoa huduma za dharula za uzazi, watoto njiti wanaozaliwa na watoto wanaozaliwa na uzito mdogo. 

Katika hatua nyingine amesema kuwa mradi huo unafadhiliwa na wadau wakubwa wawili wa maendeleo ambao ni Bloomberg Philanthropies na Gates Foundation kutoka nchini Marekani wenye ushirikiano wa muda mrefu na Serikali katika utoaji wa huduma za afya. 

Amesema kuwa kwa kushirikiana na wadau wameadhimia kufungua dirisha la kufuatilia kwa pamoja kila hatua ya utekelezaji wa mradi huo ili kuweza kuyafikia malengo yaliyowekwa ambayo ni kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.