Na WAF, Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imeridhishwa na hatua iliyofikiwa ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini hali inayo fikia asilimia 90 ya bidhaa hizo za afya.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Johannes Lukumay leo Januari 21, 2026 wakati wakipokea taarifa ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na Taasisi ya Utafiti wa Tiba (NIMR).

Dkt. Lukumay amesema jitihada zinazofanywa na taasisi hizo zina mchango mkubwa wa uboreshaji na utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.

“Pamoja na uwepo wa dawa na vifaa tiba vya kisasa, bado kuna changamoto ya uelewa mdogo kwa wananchi kuhusu teknolojia na vifaa hivyo, hali inayotokana na ukosefu wa elimu ya kutosha juu ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kwenye sekta ya afya, hivyo lazima muongeze elimu” amefafanua Dkt. Lukumay.

Katika kikao hicho, kamati pia imesisitiza umuhimu wa kuimarisha uzalishaji wa ndani wa dawa kwa kutafuta fedha za uzalishaji kupitia Taasisi ya Utafiti wa Tiba (NIMR) na kuendeleza uwezo wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ya eneo la uzalishaji, hatua ambayo itasaidia kupunguza utegemezi wa dawa kutoka nje ya nchi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI Dkt. Jafar Seif amesema Serikali inaendelea kuwekeza kwenye sekta ya afya kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na Taasisi ya Utafiti wa Tiba (NIMR) kwa lengo la kuboresha huduma za afya na kuhakikisha zinamfikia mwananchi mahali alipo.

Aidha, amesema ili kutekeleza azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imeendelea kuweka kipaumbele katika tiba asili, ambapo kwa sasa dawa za tiba asili zinapatikana ndani ya hospitali 12 za rufaa za mikoa, hatua inayochochea kupanua wigo wa huduma za afya na kumpa mwananchi wigo wa huduma.