Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amesema kuwa mfumo mpya wa usajili wa mashauri ya usuluhishi na uamuzi kwa njia ya kidijitali unaofahamika kama e-Utatuzi, unatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika utoaji wa haki nchini.
Waziri Sangu ameyasema hayo leo Januari 21, 2025, jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya kuanza rasmi matumizi ya mfumo wa e-Utatuzi.
Amesema kuwa mfumo huu utapunguza gharama za wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma katika ofisi za Tume, kuongeza uwazi na uwajibikaji, pamoja na kuchochea upatikanaji wa haki na ukuaji wa uchumi.
“Serikali inatambua umuhimu wa CMA kwa kuwa huduma zake zinagusa waajiri na waajiriwa ambao kwa msingi wao wanachangia ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. Bila CMA imara na yenye uwezo wa kutatua migogoro kwa haraka, uchumi unaweza kuathirika,” amesema Waziri Sangu.
Vilevile, ameipongeza Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kwa kazi kubwa iliyofanya kuhakikisha mfumo wa e-Utatuzi unakamilika na kuanza kutumika, akisema mfumo huo utachagiza zaidi utoaji wa haki kwa wananchi.
Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Dkt. Yose Mlyambina, amesema kuwa mfumo wa e-Utatuzi unaleta mapinduzi ya kidijitali kwa kuongeza uwazi, kasi na ufanisi katika utoaji wa haki kazi.
Naye Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Mheshimiwa Usekelege Mpulla, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwezesha usimikaji wa mfumo huo wa kidijitali, ambao utarahisisha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi kwa njia ya mtandao.





