Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Ruvuma

Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga amechangia vifaa vya ujenzi kwa Shule ya Msingi Ugano iliyopo Kata ya Kambarage na Shule ya Msingi Kibandai A iliyopo Kata ya Maguu, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma, kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Mchango huo umehusisha bati 100 za geji 28 zenye thamani ya shilingi milioni 3.5 kwa ajili ya kuezeka vyumba viwili vya madarasa, mbao za kenchi zenye thamani ya shilingi milioni 1, pamoja na mifuko ya saruji na nondo kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba katika Shule ya Msingi Ugano.

Akiwa katika Kijiji cha Kibandai A, Kata ya Maguu, Mhe. Kapinga amesema anatambua changamoto za uchakavu wa miundombinu ya shule ikiwemo madarasa, nyumba za walimu, nyumba ya mganga pamoja na ofisi za shule, na ameahidi kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kuzitatua changamoto hizo, Katika hatua hiyo, Mhe. Kapinga amechangia mifuko 50 ya saruji pamoja na shilingi laki tano kwa ajili ya ununuzi wa mchanga, ili kuharakisha ukamilishaji wa miradi ya ujenzi.

Wakati huo huo, Mhe. Kapinga amewakumbusha wananchi wa jimbo hilo umuhimu wa kujikinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa kutumia kinga na kuwa waaminifu katika mahusiano yao na kujiepusha na vitendo vyote vinavyoweza kuchangia maambukizi.


Amesema haikubaliki kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kuendelea kutajwa miongoni mwa maeneo yenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya UKIMWI kila ripoti za kitaifa zinapotolewa.

Amesisitiza umuhimu wa wananchi kuchukua hatua binafsi na za kijamii ikiwemo kupima afya mara kwa mara, kutumia kinga, na kuepuka kuwaambukiza wengine, akibainisha kuwa maambukizi ya UKIMWI hayawezi kutambulika kwa kumuangalia mtu kwa sura.

Mhe. Kapinga amemshukuru Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa miradi ya maendeleo inayoendelea katika Jimbo la Mbinga vijijini mkoani Ruvuma.

Akizungumza Dkt Salemani Jumbe Kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, amesema zaidi ya madawati 2,000 yamekamilika kutengenezwa na yako katika hatua za mwisho za kusambazwa, na yatapelekwa katika shule zote zenye upungufu wa madawati ikiwemo Shule ya Msingi Ugano, ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Dkt. Jumbe, ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, amesema Kijiji cha Kibandai A tayari kimefungua zahanati kwa ushirikiano na Mhe. Kapinga, ambaye alichangia kwa kiasi kikubwa vitanda na vifaa tiba, ameeleza kuwa kwa sasa watumishi wa afya 100 tayari wamewasili wilayani kwa ajili ya kupangiwa vituo vya kazi.

Kwa ujumla, mchango wa Mhe. Judith Kapinga umepokelewa kwa furaha na wananchi wa Kata ya Kambarage na Maguu, ambao wameeleza kuwa hatua hiyo itaongeza hamasa ya elimu, kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi, na kuonesha dhamira ya dhati ya serikali katika kuimarisha sekta ya elimu na afya.