Rais wa Marekani donald Trump amesema kuwa amefikia makubaliano ya mkakati unaomridhisha kuhusu Greenland.

Trump aliyasema hayo wakati ambapo pia amedai kuwa hatotumia nguvu kukichukua kisiwa cha Greenland na pia kudai kuwa hatoziwekea tena ushuru bidhaa za mataifa nane ya Ulaya yaliyokuwa yanaupinga mpango wake wa kuitwaa Greenland.

Akizungumza na kituo cha habari cha Marekani CNBC,Trump alisema makubaliano hayo ni ya muda mrefu na kila mmoja ameyafurahia ila hakutoa taarifa zaidi na hakusema pia iwapo hiyo inamaanisha kuwa Marekani itakuwa na udhibiti wa kisiwa hicho cha eneo la Arctic.

Trump aliyasema yote hayo baada ya mkutano huko Davos na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Mark Rutte ambaye kupitia msemaji wake, ameyathibitisha hayo aliyoyasema Trump.

Lakini waziri wa fedha wa Ujerumani Lars Klingbeil ameonya dhidi ya kuwepo kwa matumaini ya mapema kutokana na hiyo kauli ya Trump kuwa sasa hatoziwekea tena bidhaa za Ulaya ushuru.

Vitisho vya Trump vilikuwa vimezusha mmojawapo wa mizozo mikubwa zaidi katika eneo la transatlantic kuwahi kushuhudiwa kwa miongo kadhaa, akisema kwamba anaweza kuisambaratisha NATO.