Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Crispin Francis Chalamila, amekabidhi mashine mbili za kuwahudumia watoto waliozaliwa kabla ya muda (watoto njiti) kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani (Tumbi), ikiwa ni sehemu ya matendo ya huruma yanayofanywa na watumishi wa taasisi hiyo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika Januari Chalamila amesema mashine hizo zimepatikana kupitia michango ya watumishi wa TAKUKURU kutoka mikoa yote nchini, lengo likiwa ni kusaidia jamii kwa kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda.
“Mashine hizi ni matokeo ya michango ya watumishi wa TAKUKURU nchi nzima kama sehemu ya kujitoa kwao kwa jamii. Dhamira yetu ni kuhakikisha kila Mkoa Tanzania Bara unapata msaada huu,” amesema Bw. Chalamila.
Kwa upande wake, Dkt. Adelina Rutashobya, Daktari Bingwa wa Watoto katika Hospitali ya Tumbi, amesema takwimu zinaonesha kuwa asilimia 16 ya watoto wanaopokelewa hospitalini hapo hupoteza maisha, hali inayosababishwa kwa kiasi kikubwa na uhaba wa vifaa tiba hususan kwa watoto wanaozaliwa chini ya wiki 28.
Amesema ujio wa mashine hizo mbili utaongeza uwezo wa hospitali hiyo katika kuwahudumia watoto njiti na hivyo kupunguza vifo vinavyotokana na changamoto za vifaa tiba.
Naye Dkt. Amani Malima, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Pwani (Tumbi), ameishukuru TAKUKURU kwa msaada huo akisema utakuwa na mchango mkubwa katika kuokoa maisha ya watoto wengi wenye uhitaji.
“Kwa kiasi kikubwa mashine hizi tulizozipokea kutoka kwa watumishi wa TAKUKURU zitaokoa maisha ya watoto wengi. Tunawashukuru sana kwa moyo wao wa kujitoa,” amesema Dkt. Malima.
Awali, Bw. Chalamila alieleza kuwa mpango huo ulianza Desemba 2024 mkoani Arusha, ambako TAKUKURU ilitoa msaada wa mashine hizo kwa mara ya kwanza, hatua iliyowapa hamasa ya kuendeleza matendo ya huruma kwa kuwafikia watoto nchi nzima kupitia hospitali za rufaa za mikoa.
Hadi sasa, TAKUKURU tayari imekabidhi mashine za watoto njiti katika mikoa tisa (9) ambayo ni Arusha, Ruvuma, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Manyara, Dodoma na Pwani.



