Na Farida Ramadhani na Joseph Mahumi, WF, Dodoma
Serikali na GATSBY Africa wamejadiliana vipaumbele vya Tanzania katika mabadiliko ya kiuchumi hasa katika kuimarisha ushindani wa uzalishaji wa viwanda ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa 2050.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa GATSBY Africa, Bw. Justin Highstead aliyeambatana na wajumbe wengine kutoka Taasisi hiyo.
Alisema majadiliano hayo yanalenga vipaumbele vya nchi ambavyo vimeanishishwa katika Dira ya Taifa 2050 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa miaka 5 na vinapaswa kutekelezwa ili kufikia lengo la taifa.
“Hapa katikati katika utekelezaji Dira ya Taifa 2050 na Mpango wa Maendeleo, tumeangalia kwa pamoja, mageuzi ya kiuchumi kwanza ambapo ndani yake kuna ya mapinduzi ya viwanda, uwekezaji mkubwa wa kifedha pamoja na uwekezaji mkubwa wa kujenga rasilimali watu”, alisema Mhe. Balozi Omar.
Aliongeza kuwa katika kikao hicho walijadiliana pia masuala ya sayansi na teknolojia, utafiti pamoja na utafutaji wa rasilimali kwa ajili ya utekelezaji wa vipaumbele hivyo ambapo baadae wataangalia namna bora ya kushirikiana katika utekelezaji.
Aidha, aliipongeza taasisi hiyo kwa ushirikiano ambao imekuwa ikitoa hususan ushirikiano na Tume ya Mipango katika kuandaa tafiti na uchambuzi unaosaidia utekelezaji wa dira na mipango ya maendeleo ya Taifa na maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa GATSBY Africa, Bw. Justin Highstead, alisema taasisi hiyo inafanya kazi Afrika Mashariki kwa ujumla, hasa Tanzania kwa zaidi ya miaka 25 na inalenga mageuzi ya kiuchumi na kusaidia mabadiliko ya sekta mbalimbali za uchumi.
Alisema kazi wanazofanya zinahusisha ushirikiano wa karibu na Serikali, pamoja na sekta binafsi, ili kusaidia juhudi za Serikali katika kukuza uchumi na kuendeleza sekta zenye uwezo wa kubadilisha uchumi wa nchi.
Bw. Highstead alibainisha kuwa kwasasa wanajihusisha na misitu na kilimo na kwamba wapo tayari kushirikiana na Serikali katika kuangalia sekta nyingine zenye fursa kubwa za mageuzi ya kiuchumi.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, Kaimu Kamishna wa Idara ya uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha, Dkt. Remidius Ruhinduka, Kamishna Msaidizi wa Idara ya uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha, Bw. William Mhoja, na maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha na Taasisi ya GATSBY Africa.






(Picha na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Fedha)


